March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yachanja mbuga na ‘Anzia Ulipo’ Kanda ya Kusini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Mawasiliano inayoongoza hapa nchini, Yas imeendeleza Kampeni yake mpya ya ‘Anzia Ulipo’ kupitia uzinduzi uliofanyika jijini Mbeya.

Hatua hiyo inalenga kuhimiza wakazi wa Kanda ya Kusini na Watanzania kwa ujumla kuanza safari ya mafanikio kutoka pale walipo kwa kutumia teknolojia na huduma bunifu za kisasa za Yas.

Uzinduzi huo umefanyika mwishoni mwa juma katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa biashara, wafanyakazi wa Yas na Mixx pamoja na wakazi wa Mbeya.

Katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kusini, Abbas Abdurahamani, ambaye alielezea kampeni hiyo kama chachu ya mabadiliko ya kweli katika maisha ya Watanzania.

“Kampeni ya Anzia Ulipo si tu kauli mbiu bali ni falsafa inayohamasisha kila Mtanzania kutumia kile alichonacho kuanza safari ya mafanikio.

Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kusini Abbas Abdurahamani (katikati), Mkurugenzi wa Masoko Edwardina Mgendi (kulia), na Meneja wa Masoko ya Biashara, Saumu Mwekijazi (kushoto) wakifurahia wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Anzia Ulipo” katika Kanda ya Kusini, iliyofanyika jijini Mbeya, Juni 20 mwaka huu.

“Yas inatoa miundombinu ya kisasa, huduma bora, na mtandao wa kasi unaofika kila kona ya nchi ili kuwezesha hilo,” amesema Abdurahamani.

Akitumia mifano ya maisha halisi, Abdurahamani amesisitiza kuwa kupitia uwekezaji mkubwa wa Yas katika mtandao wa 4G na 5G, sasa wakulima wanaweza kupata taarifa za soko kwa wakati, walimu kufundisha mtandaoni, na wajasiriamali kuuza bidhaa zao hata nje ya mipaka ya nchi.

“Leo hii, kutoka Tukuyu hadi Uyole, Mtanzania anaweza kuendesha biashara kidijitali, kujifunza, na kutimiza ndoto kupitia mtandao wa Yas,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Yas Tanzania, Edwardina Mgendi ameeleza kuwa kampeni ya ‘Anzia Ulipo’ ni majibu kwa changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowakabili Watanzania wengi hasa vijana.

“Nguvu ya mabadiliko haiko kesho, iko kwenye hatua tunazochukua leo. Tunataka kila mmoja ajue kuwa mafanikio yanaanzia pale alipo, iwe kijijini, mjini, kazini au sokoni. Yas ni mshirika wa kweli katika safari hiyo,” amesema Mgendi.

Edwardina amebainisha kuwa hadi sasa, Yas imefanikiwa kufikisha mtandao wa 4G kwa zaidi ya asilimia 95 ya nchi na inaendelea kusambaza 5G kwa kasi, jambo linalofungua milango ya ajira, elimu, biashara na ubunifu kwa mamilioni ya Watanzania.

Mbali na uzinduzi rasmi, Kampeni ya ‘Anzia Ulipo’ inatarajiwa kuendelea na shughuli mbalimbali za kitaifa zikiwemo vipindi vya redio, kampeni za mitandaoni, mafunzo ya kidijitali, na kushirikiana na wajasiriamali wadogo ili kuwajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo.

Kwa mujibu wa viongozi wa Yas, Mbeya imechaguliwa kama kituo cha uzinduzi kutokana na historia yake ya ubunifu, ujasiriamali na maendeleo ya kijamii.

Kampeni hiyo inatarajiwa kupenya hadi maeneo ya vijijini ili kuhakikisha Watanzania wote wanagusa faida za dunia ya kisasa ya kidijitali.

“Hatuzungumzii tena miundombinu tu, tunazungumzia daraja la fursa. Yas ipo kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,” amesisitiza Abdurahamani.