Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza
Imeelezwa kuwa licha ya uwepo wa sheria na sera,bado ukatili dhidi ya watoto unaendelea kwenye familia,shuleni na jamii,ikiwemo baadhi ya wazazi na walezi,kutotekeleza wajibu wao wa malezi chanya na ulinzi wa watoto.
Huku changamoto ikiwa ni mimba na ndoa za utotoni hasa maeneo ya vijijini,kuongezeka kwa watoto wanaoishi na walioko katika mazingira hatarishi, kukosa ulinzi na huduma muhimu.

Kufuatia hali hiyo,watoto wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza,wametoa wito kwa Serikali,kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu malezi bora ya watoto.
Akisoma risala ya watoto wa Wilaya ya Nyamagana,Mwanahabari Mtoto kutoka shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza(MYCN), Brightness Boniface,katika siku ya maadhimisho ya Mtoto wa Afrika,ambayo ufanyika kila Juni 16 ya kila mwaka,ambapo kiwilaya yamefanyika mtaa wa Kishili A,jijini Mwanza.
Brightness ameeleza kuwa,lengo la elimu kutolewa kwa wazazi na walezi ni waweze kuwajibika ipasavyo katika kuwalinda,kuwatunza na kuwaendeleza watoto wao kwa upendo,uelewa na uwajibikaji wa pamoja.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,Ofisa Elimu Taaluma wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,Julius Magembe, amewataka wazazi kuhakikisha wanatekeleza haki za watoto,ikiwemo kuwalinda,kuwaendeleza,kuwasikiliza na kuwashirikisha.
Huku akionya,wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto, katika biashara mbalimbali ikiwemo za kuuza karanga na usambazaji wa vyakula kwa wanaofanya shughuli za mama lishe, na badala yake wawapeleke shuleni kupata elimu.
“Ndoto za watoto zinaweza kuwa kweli endapo wazazi watahakikisha wanatimiza wajibu wao,kwa kuwalinda,kuwaelekeza wajibu wao, kuwasikiliza na kuwashirikisha.Tuwalinde na kuwatunza watoto wetu,”amesema Magembe.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa Vijana, Elimu,Malezi na Ajira (VEMA)kutoka shirika la Plan International,Gadiel Kayanda, amesema,ili kukomesha vitendo vya kikatili kwa watoto,elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwani kujifunza hakuna mwisho na ndio njia sahihi ya kumaliza tatizo.
“Waswahili wanasema,elimu haina mwisho kwaio tuendelee kuhamasisha,kufundishana,kuelekezana,kukumbushana,kuelimishana kuhusu ukatili ni nini,na wapi tunapaswa kutoa taarifa.Naamini tukifanikiwa kutoa elimu cha kwanza tutakuwa tumekomboa fikra za watu wengi kuhusu ukatili,” amesema Kayanda.

Amesema,hatua nyingine ni kuhakikisha wadau wote wanashikamana, kwani serikali au shirika moja haliwezi kukomesha ukatili pekee yake,pia wazazi,walezi na jamii kuwekeza katika kuwalea watoto kwa usahihi.
Mmoja wa wazazi wilayani Nyamagana,Witness Elias,amesema,ni vyema elimu ikatolewa mara kwa mara kwa wazazi na walezi kuhusu ukatili na masuala yote yanayohusu watoto.

More Stories
REA yaendelea kusambaza Nishati Bora kwa wananchi,yamshukuru Rais Dkt.Samia
Vivo Energy Tanzania, yazindua Kampeni ya “Uliza Oili ya Shell”
Kampeni ya kisheria ya Mama Samia kuondoa migogoro na ukatili