Asema Serikali imeamua kuliinua zao hilo ili kukuza uchumi
Na.Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Simiyu
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua viwanda viwili cha pamba na mabomba mkoani Simiyu huku akisisitiza kuwa, Serikali imedhamiria kufanya uwekezaji katika zao hilo na mabadiliko yake yataonekana taratibu kwa kukuza uchumi wa nchi, mkoa na watu.
Rais Dkt. Samia amesema hayo katika ziara yake mkoani Simiyu wakati akizindua viwanda hivyo viwili ambavyo ni kiwanda cha kuchakata mabomba pamoja na kiwanda cha kuchakata pamba, wilayani Bariadi, ambapo amekiri kuridhishwa na uchakataji wa zao la pamba katika kiwanda hicho.

Pia amesema, ameridhika na maelezo yaliotolewa na Waziri wa Kilimo,Hussein Bashe, mara baada ya kuwasili mkoani humo hivyo anatoa wito kwa wananchi kuwa tayari na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya kilimo.Hivyo wakulima wa pamba wakae mguu sawa.
Rais Dkt. Samia,amesema, mabadiliko hayaji mara moja ni hatua na yana maumivu lakini watakaoumia si wakulima bali waliozoea kuwalalia wakulima kwa kununua pamba kwa bei ya chini.
“Nawashukuru wananchi kwa mapokezi.
Nimefungua kiwanda hiki cha mabomba na kuchakata pamba, nimeona kazi inayofanywa na
ubora wake nimejiridhisha, hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni katika zao la pamba,”amesema.
Amesisitiza kuwa, kama ambavyo nchi imefanya vizuri katika zao la korosho, kahawa, tumbaku, mbaazi ndivyo ambavyo serikali inaenda kuweka nguvu katika kulipandisha zao la pamba.
“Uzalishaji wa mabomba utatusaidia,kwani tunayo miradi mingi ya usambazaji maji,”amesema Dkt.Samia na kuongeza:
“Tukiwa na wazee jana jioni Waziri wa Kilimo alitueleza mengi,mipango ya Serikali katika kuliwezesha zao hili la pamba, tumepandisha zao moja moja sasa tumegeukia pamba hatua tunazochukua ni kwa faida yetu, mabadiliko yanakuwa na maumivu kidogo watakaoumia ni wale ambao hawalimi wanaonunua mazao kwa kuwalalia wakulima na hao ndio wanakuwa na kelele,”.

Alisema, mwekezaji wa kiwanda hicho amewaza vyema na ataungana na Serikali kuhakikisha nchi inasitisha upelekaji malighafi za pamba na kuitengeneza hapa hapa nchini ili watu wapate ajira.
“Hicho ndicho tunachotaka, Watanzania wenye uwezo wawekeze hapa na kukuza uchumi wetu sisi wenyewe niwaombe wafanyabiashara wengine wafanye jitihada za uwekezaji.
Serikali imefanya kazi nzuri za maendeleo na zinaonekana wekezeni nyumbani,”alisema.
Viwanda hivyo vyenye thamani ya Sh. bilioni 8, vinamilikiwa na Kampuni ya Moli Oil mills company LTD, ambao pia ni wamiliki wa kampuni za Nsagali.
Aidha viwanda hivyo vimezalisha takribani ajira 850 za moja kwa moja, pamoja na ajira nyingine 400, huku vikitoa fursa kwa wajasiriamali wadogo wadogo kunufaika kwa kufanya biashara za mama lishe.
Rais Dkt. Samia yuko katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, hadi Juni 19, mwaka huu.

More Stories
Simbachawene aipa tano Tume ya madini
TANAPA kunadi maeneo yake ya uwekezaji Zanzibar
Waziri Mavunde ataka watanzania kupewa kipaumbele kusambaza bidhaa na huduma migodini