Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
KATIKA mwaka wa fedha 2024/25, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kwa kushirikiana na taasisi zake, wadau wa maendeleo, na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, imeweka msukumo mpya katika kuhakikisha jamii inakuwa kitovu cha maendeleo kwa kuimarisha ushiriki, fikra sahihi, na maadili mema.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma, wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025, Waziri wa Maendeleo ya Jamii ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesema, Serikali imeendelea kusimamia kwa karibu Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha Maendeleo katika Ngazi ya Msingi (2022/23 – 2025/26) unaolenga kuchochea mabadiliko ya kifikra na kuongeza ufanisi wa huduma za kijamii nchini.
“Mheshimiwa Spika, kupitia mpango huu, wananchi wanahamasishwa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zao,tumeweza kuwahusisha wananchi katika utekelezaji wa miradi 31,802 ya maendeleo kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara,” alisema Waziri.
Katika hatua nyingine Dkt.Gwajima amesema , Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuendeleza maadili na utamaduni wa Mtanzania, kama nguzo muhimu ya maendeleo ya jamii.
Amesema,ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili, Wizara imeandaa Kitini cha Uwezeshaji wa Majadiliano ya Mila na Desturi Ngazi ya Jamii, ambacho kinatumika kama nyenzo ya kutoa elimu na uhamasishaji kwa jamii kuhusu matumizi chanya ya mila na desturi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo,jumla ya wananchi 20,211 kutoka mikoa ya Mwanza, Mara na Tabora wameshiriki katika mijadala hiyo ya kijamii, hatua inayoelezwa kuwa ni msingi wa kujenga jamii inayojitambua na kujenga taifa lenye maadili thabiti.
“Mheshimiwa Spika, maadili bora hujengwa kutoka ngazi ya familia hadi taifa. Ndiyo maana tunaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na sekta nyingine ili kuhakikisha jamii inayaishi maadili haya kwa vitendo,” aliongeza.
Aidha, katika kuendeleza elimu ya kijamii amesema,Serikali inaendelea kusimamia vyuo 8 vya Maendeleo ya Jamii nchini, ambavyo ni pamoja na vyuo vya Ruaha, Rungemba, Uyole, Mlale, Monduli, Buhare na Mabughai na Misungwi.
“ Vyuo hivi vinatoa mafunzo kwa watalaam wanaotumika kama daraja kati ya Serikali na jamii katika kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo.”amesisitiza
More Stories
DC Ubungo kuanza kuwasajili ‘bodaboda’
NEC yachagua wajumbe wa kamati kuu,yumo Asas
Waziri Aweso atoa maelekezo kwa Wakurugenzi huduma za maji nchini