May 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Thabo Mbeki aipongeza Tanzania kuandaa mhadhara wa UNISA mara tatu mfululizo

Na Penina Malundo,Timesmajira

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki ameipongeza taifa la Tanzania  kuwa nchi pekee kuwahi kuandaa mhadhara wa Thabo Mbeki wa Siku ya Afrika mara tatu  jambo linalodhihirisha dhamira yake ya dhati kwa mshikamano na maendeleo ya Afrika.

Akitoa pongezi hizo jana wakati wa Mhadhara huo uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) amesema tangu enzi za Marehemu Hayati  Rais Benjamin Mkapa hadi sasa, Tanzania imekuwa ikionyesha uongozi dhabiti katika mijadala ya maendeleo ya bara. 

Amesema hii inaonyesha ubora wa uongozi na maono ya taifa hili,licha ya  mihadhara mingi kati ya 15 imefanyika Afrika Kusini, nia ni kuihamishia kwenye mataifa mbalimbali ya Afrika.

“Ningependa kutoa shukrani za dhati kwa  Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuturuhusu kukutana na kuandaa mhadhara huu hapa Tanzania ambao umewaleta  viongozi, wasomi na wadau kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na nje ya bara,  kwa lengo la jukumu la  kusaidia kuelekeza mustakabali wa Afrika,”amesema.

Aidha Rais huyo wa zamani ameelezea kuhusu chimbuko la Taasis ya Thabo Mbeki na dhamira yake ya kushughulikia changamoto zinazoendelea kuikabili Afrika, hususan ukosefu wa utekelezaji wa sera nzuri zilizopitishwa.

“Wenzangu waliniambia kabla sijastaafu mwaka 2008 kwamba niendelee kujikita katika changamoto za Afrika. Tumepitisha sera nzuri kote barani, lakini kuna watu wachache sana wenye uwezo wa kuzitekeleza,” amesema.

Ili kushughulikia pengo hilo, Mbeki amesema kuwa mojawapo ya hatua za mwanzo za taasisi yake ilikuwa ni kuanzisha Shule ya Uongozi Afrika, na baadaye Taasisi ya Kiafrika ya Thabo Mbeki katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA), taasisi ya masomo kwa umbali yenye mtandao mpana barani Afrika inayowahudumia wanafunzi kutoka zaidi ya nchi 40 za Afrika.

“Lengo lilikuwa kujenga mtaji wa watu—viongozi wa baadaye watakaosukuma mbele maendeleo ya Afrika,” alifafanua. “Haikuwa kuhusu Afrika Kusini pekee. Hii ni taasisi ya Afrika yenye dhamira ya bara zima.”amesema