Na Penina Malundo ,Timesmajira
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo, wakizingatia viapo vyao kwa vitendo.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni katika hafla iliyofanyika Ikulu, ambayo pia ilihusisha kiapo cha maadili kwa viongozi waliokwishateuliwa siku za nyuma.
Viongozi walioapishwa ni Prof. Tumaini Joseph Nagu aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya afya; Dkt. Blandina Buganzi Kilama aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu na Jaji Mstaafu John Samweli Mgetta aliyeteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili.

Rais Dkt. Samia amewataka viongozi hao kushirikiana kikamilifu katika kazi na watumishi wa ofisi wanazokwenda, kuheshimu maadili ya utumishi wa umma na kuwa mfano wa uongozi bora kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Kadhalika, Rais Dkt. Samia amewaagiza viongozi wa Tume ya Mipango kushirikiana katika uratibu wa miradi mikubwa ya kitaifa na kuhakikisha kuwa inafungamana na malengo ya kitaifa.

Kwa upande wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Rais Dkt. Samia amelielekeza Shirika hilo kuendeleza vyanzo vidogovidogo vya uzalishaji umeme nchini, kusimamia usambazaji wa umeme wa uhakika unaozalishwa pamoja na kutathmini uzalishaji umeme kwa vyanzo vya nishati jadidifu.
More Stories
TAZAMA PIPELINE yalishika mkono jeshi la polisi Mbeya
Vyama vya Ushirika Katavi vyatakiwa kuthibiti utoroshaji mazao
Suluhu mgawanyo wa mapato wa huduma za usafiri wa anga nchini, wapatikana