May 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jukwaa la Maendeleo Katavi lasaidia mahitaji ya Mil.5.7 kituo cha watoto yatima,mahabusu

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.

JUKWAA la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Katavi limetoa mahitaji mbalimbali yenye thamani ya fedha zaidi ya Mil 5.7 katika kituo cha kulelea Watoto yatima na waishio mazingira magumu cha Mt.Yohane Paul II na Gereza la Mahabusu Mpanda.

Utoaji wa mahitaji hayo ni sehemu ya utekelezaji msingi saba ya ushirika ulimwenguni unaowataka kama wanaushirika katika shughuli zao za kiuchumi wanazozifanya kurudisha sehemu ya kile wanachokipata kwa jamii.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Peter Nyakunga akizungumza Mei 22, 2025 katika kituo cha Mt.Yohane Paul II wakati wa maadhimisho ya siku ya jukwaa la ushirika utakao fanyika kwa siku mbili amesema kwa kuwa ushirika unawahusu watu wengi hivyo wanawajibika kurudi kwa jamii na kuisaidia.

Nyakungu amebainisha katika kituo cha Mt. Yohane Paul II licha ya Kwenda kuwapatia tabasamu wameweza pia kutoa mahitaji yenye thamani ya mil 1.8 huku katika gereza la mahabusu Mpanda wakitoa mahitaji yenye thamani ya mil 3.97.

Mrajisi huyo ameweka wazi kuwa mambo mengine yaliyofanyika katika jukwa la ushirika katika ukumbi wa Mpanda Social Hall ni kutolewa kwa mada mbalimbali na wataalamu kwa ajili ya kuwapatia elimu wanaushirika.

Elimu walizopata ni pamoja na kufahamu umuhimu wa kuwa na akauti benki, masuala ya kikodi, bima za afya kwa wanaushirika na kufahamu umuhimu wa kujiunga na mfuko wa kijamii wa NSSF.

“Michango ya jamii kupitia NSSF ni muhimu kwa wanaushirika kujiunga kwani shughuli zao za kilimo wanaweza kuzifanya katika umri fulani kati ya miaka 50 hadi 60 lakini baada ya nguvu zao kwisha hawataweza kufanya kilimo na badala yake wanaweza kunufaika na mafao” Amesema Nyakunga.

Mwenyekiti wa Chama Cha Ushirika Mkoa wa Katavi, Amosi Kaega amesema kuwa furaha ya kutembelea maeneo ya watu wenye uhitaji hususani kituo cha kulelea Watoto yatima kwani wanahitaji shughuli za kila siku za wanaushirika kuweza kuwasaidia kama sehemu ya utekelezaji wa mambo saba ya wanaushirika.

“Vitu tulivyonunua na kupeleka katika kituo hicho ni mchele kg 200, maharagwe kg 200 na vitu vingi ambavyo tumekabidhi mahala hapo” Amesema Kaega.

Vilevile Mwenyekiti huyo wa Ushirika amesema wamechagua kutoa mahitaji katika gereza la mahabusu Mpanda kwa sababu gereza linaweka watu mbalimbali wenye makosa na wasio na makosa wakiwemo na wanaushirika humo ndani.

Amesema baada ya kufika mahala hapo waliona ujenzi wa upanuzi wa mahabusu ambapo waliamua kununua mifuko 50 ya cementi, nondo 60 na vitu vidogovidogo kwa ajili ya kuhakikisha  ujenzi huo unakamilika kwa haraka.

Mlezi kiongozi wa Kituo cha Mt. Yohane Paul ii, Veronica Sungura anamshukuru Mungu kwa kuwajalia Watoto wanaoishi kwenye kituo hicho afya njema na kuwajalia watu wanaoona umuhimu wa kuwasaidia watoto hao.

“Ni Mungu anaweka ndani yenu nguvu na neema ya kutambua uhitaji na mahitaji muhimu ya hawa Watoto na mkafikiri kwamba ni vema kuwatembelea, ni vema kuwapelekee chochote na vema Kwenda kuunga mkono viongozi wa kituo hiki kwa kazi hii wanayoifanya ya jamii” Amesema Veronica.

Aidha ametoa shukrani Wanaushirika Mkoa wa Katavi kwa kufanya mambo mengi yanayohusu jamii na kile wanachokipata kuona kheri ya kurudisha shukrani kwa Mungu kupitia Watoto hao.