Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Yas imeungana na Kampuni ya Redington, ambao ni wasambazaji waliothibitishwa wa bidhaa za Apple hapa nchini, kwa ajili ya kusambaza simu mpya ya iPhone 16E katika maduka yote ya Yas nchi nzima.
Kupitia ushirikiano huo, Watanzania sasa wataweza kupata iPhone 16E iliyounganishwa na kifurushi cha intaneti cha bure cha GB 96 kwa mwaka mzima na chaja ya bure ya wati 20.
Lengo la kufanya hivyo ni, kumuongezea mteja thamani na kumwezesha kuanza kutumia simu hiyo papo hapo bila shida yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, wakati wa hafla hiyo, Meneja wa Huduma za Vijana na Wateja Maalum Yas, Ikunda Ngowi alisema ushirikano huo ni sehemu ya mkakati wa Yas wa kuendelea kuwawezesha Watanzania kidigitali kwa kuendelea kuja na mikakati ya kibunifu kila siku.
“Yas tunajivunia kuwa kinara wa uwezeshaji kidijitali nchini kwa kuendelea kutoa huduma za kibunifu zinazoendana na mahitaji halisi ya Watanzania katika maisha yao ya kila siku.
“Uamuzi wetu wa kushirikiana na Kampuni ya Redington kuleta huduma hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuwafikia wapenzi wa simu aina ya iPhone, pamoja na kukuza uwepo wetu katika soko la simu aina ya Iphone linalokua polepole.

“Kwa mujibu wa Ripoti ya Statcounter Globalstat ya Machi 2025 ni asilimia 6.49 tu ya Watanzania ndio wanatumia simu za iPhone,” alisema Ngowi.
Kwa upande wake, Eric Mkomoye, Meneja wa Mauzo wa Redington Tanzania, alisema ushirikiano huu unaendana na lengo la Redington la kuhakikisha teknolojia bora duniani inawafikia watu wengi zaidi Afrika.
“Tunajivunia kushirikiana na Yas katika kuhakikisha iPhone 16E inawafikia Watanzania kwa urahisi.
“Kama wasambazaji waliothibitishwa wa Apple, tunahakikisha wateja wanapata bidhaa halisi kupitia washirika wa kuaminika, pamoja na huduma bora.

“iPhone 16E ni simu yenye uwezo mkubwa yenye teknolojia mpya ya akili Mnemba, ina mega pixel 48, haiingizi maji na moja ya toleo bora kabisa kwenye 16 series kutoka Apple”. alisema Mkomoye.
Yas inaendelea kuweka historia kama Kampuni ya kwanza ya Mawasiliano nchini kushirikiana na msambazaji rasmi wa bidhaa za Apple kuleta toleo jipya la iPhone 16E moja kwa moja katika maduka yake.
Jambo hilo linaloendelea kuifanya kuwa kinara wa mabadiliko ya kidijitali hapa nchini.


More Stories
Jiji la Dar-es-Salaam latenga bilioni 18 za mkopo wa asilimia 10
Yas yatoa msaada wa vifaa Hospitali ya Bombo Tanga
Aweso:Rais Samia ameweza kumtua mwanamke ndoo kichwani