Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Dar
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Flaviana Matata Foundation(FMF),limesema jamii bado inahitaji kupata elimu zaidi ya masuala ya Afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia.
Hivyo FMF imeviomba vyombo vya habari nchini kuendelea kusisitiza na kutilia mkazo masuala hayo.
Hayo yamebainishwa jijini hapa leo Mei 22,2025 na Ofisa Miradi wa Shirika la FMF,Suzan Cleophas katika mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kuhusu masuala ya afya uzazi na ukatili wa kijinsia chini ya ufadhili wa Women Fund Trust.
Amesema licha ya matukio ya ukatili wa Kijinsia kupungua bado elimu inahitajika zaidi katika jamii.
“Sisi peke yetu FMF hatutoshi lakini tukiungana kwa pamoja Serikali na wadau wengine kuhakikisha elimu inafika na kuhakikisha matukio ya ukatili yanapungua na kuisha kabisa,”amesema.
Amesema FMF imekuwa ikiamini kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikifanya kazi kubwa sana hivyo kupitia mafunzo waliyoyatoa kwa waandishi wa habari jamii itapata ujumbe.
Aidha amesema Shirika hilo limekuwa likifanya kazi katika Mkoa wa Shinyanga,Pwani , Njombe, Ruvuma na Mwanza kutokana na takwimu zilizotolewa na Serikali na kuamua kwenda kutoa elimu kutokana na uwepo wa matukio ya ukatili.
“Tumekuwa tukifanya kazi katika mikoa hiyo kupitia mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2023 hadi 2027″amesema.
Awali Mwezeshaji wa mafunzo ya stadi za Maisha Kitaifa, Rehema Longo ameipongeza FMF kwa kuamua kuiunga mkono Serikali katika kuelimisha watu juu stadi za maisha.
Aidha amewaomba waandishi wa habari kupitia mafunzo hayo waliyoyapata kuwa mabalozi wazuri kwa kuifikisha elimu hiyo katika jamii.
Longo amesema ukatili, unyanyasaji na uzalishaji umekuwa ukifanyika katika jamii hivyo amewataka waandishi wa habari kwenda kuibua vitendo hivyo.




More Stories
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi