Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
JESHI la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia wanawake wawili wakazi wa Jijini hapa kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilogramu 320.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya,Benjamin Kuzaga Mei,21,2025 amewataja watuhumiwa hao kuwa ni ,Seva Simwinga (29) na Sara Simwinga (35) ambao wote ni wafanyabiashara wakazi wa Mponja ,Uyole Jijini Mbeya.
Aidha Kuzaga amesema watuhumiwa walikamatwa Mei 21, 2025 majira ya usiku katika operesheni maalum iliyofanywa na Jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya huko katika Mtaa wa Mponja uliopo Kata ya Uyole, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya.

Ameeleza kuwa watuhumiwa hao walikutwa na magunia 4 na masanduku 4 yenye dawa hizo za kulevya wakiwa wamehifadhi ndani ya nyumba wanamoishi.
Pamoja na hilo Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa pia Jeshi la polisi Mbeya linawashikilia Billy Mtafya [19] fundi magari, mkazi wa Uyole Jijini Mbeya na Joseph Nyalusi [25] kondakta wa Basi, mkazi wa Dodoma wakiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi yenye uzito wa Kilogram 30.
Amesema watuhumiwa walikamatwa kati ya Mei 19 – 20, 2025 saa 8 usiku katika kizuizi cha Polisi kilichopo katika eneo la Mpakani katika barabara kuu ya Mbeya Njombe Wilayani Mbarali wakiwa na mabegi manne na sanduku moja yakiwa yamefungwa na mifuko ya nylon ndani yake yakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi wakisafirisha kama mzigo katika Mabasi ya abiria yenye namba za usajili T.683 ELK aina Yutong mali ya kampuni ya ABC Upper Class na Basi namba T.385 EEU aina ya Yutong mali ya kampuni ya Shabiby Class yaliyokuwa yakitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kamanda Benjamin Kuzaga, linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani haina nafasi katika jamii na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lipo makini kuwabaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na biashara hiyo. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa jamii kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

More Stories
TCM,VETA zasaidia vijana 1500 kufanya kazi migodini
FMF:Taifa bado linahitaji elimu masuala ya afya ya uzazi
Dkt.Tax:Vyombo vya usalama vinaendelea kuchukua tahadhari ,Taifa lipo salama