Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Serikali kupitia Wakala wa Vipimo (WMA) nchini imekagua na kuhakiki vipimo 1,013,859 ambavyo ni sawa na asilimia 99.2 ya lengo la kukagua vipimo 1,022,342 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amebainisha hayo bungeni Dodoma leo, Mei 14, 2025 wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Kati ya vipimo vilivyokaguliwa na kuhakikiwa, vipimo 10,898 vilirekebishwa na 761 vilikataliwa,” amesema.
Aidha, Waziri Jafo ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2024/2025, Wizara yake kupitia WMA iliendelea kufanya kaguzi za kawaida na kaguzi za kushtukiza ambapo jumla ya kaguzi 3,293 kati ya 3,000 zilizopangwa kufanyika kwa vipimo mbalimbali vitumikavyo kwenye biashara, afya, usalama na mazingira zimefanyika, sawa na asilimia 109.8

Akifafanua, amesema kuwa vipimo vilivyokaguliwa kwa wingi ni pampu za kuuzia mafuta ya nishati, Flowmeters ambazo hutumika kupimia mafuta kwenye bohari na maghala ya kuhifadhia mafuta,.
Vingine ni tenki za kuhifadhia na kusafirishia mafuta, dira za maji, mizani inayotumika kupimia bidhaa mbalimbali, vipimo vya urefu pamoja na malori yabebayo kokoto, mchanga na vifusi.
Akizungumzia udhibiti wa bidhaa zilizofungashwa, Waziri Jafo ameeleza kuwa hadi kufikia Machi 2025, WMA imefanya kazi hiyo katika vituo 13 kwenye maeneo ya mipakani na bandarini.
Amevitaja vituo hivyo kuwa ni Sirari (Mara), Mtukula (Kagera), Namanga (Arusha), Holili (Kilimanjaro), Tunduma (Songwe), Tarakea (Kilimanjaro) na Horohoro (Tanga).
Vingine ni Kasumalu (Mbeya), Kwara na Bagamoyo (Pwani), Manyovu (Kigoma) na Mbweni pamoja na Temeke (Dar es Salaam).
Ametaja baadhi ya bidhaa zilizokaguliwa kuwa ni mbao, mbegu za mimea, mafuta ya kula, sabuni, maziwa, matunda, sukari, dawa ya meno, chumvi, vinywaji vya pombe, mbolea, vifaa vya ujenzi, gesi, waya na maji.
Bunge limepitisha maombi ya shilingi 135,788,232,000 kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi 93,900,697,000 ni kwa matumizi ya kawaida na shilingi 41,887,535,000 ni kwa matumizi ya maendeleo.
More Stories
Mke wa Rais wa Finland atembelea Makumbusho ya Taifa
Lulida ataka viwanda vilivyofungwa vifufuliwe
Rais Mwinyi:Tutamuenzi Charles Hilary kwa utendaji wake uliotukuka