Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa UshetuEmmanuel Cherehani amekataa majibu ya serikali ya kumalizika kwa mgogoro wa mipaka uliopo kati ya mkoa wa Shinyanga (Ushetu) na Tabora (Kaliua).
Hayo yamejiri Bungeni Jijini jana katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni ambapo katika swali lake la msingi Mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka wa Shinyanga na Tabora katika eneo la Ushetu na Kaliua ambao umechukua muda mrefu sana.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zainabu Katimba , kwa mujibu wa Tafsiri ya ardhini ya Matangazo ya Serikali ya uanzishwaji wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga na Kaliua Mkoani Tabora hakuna mgogoro wa mpaka kati ya mikoa hiyo miwili.
Alisema,mgogoro uliopo wa mpaka ni kati ya Hifadhi ya Msitu wa Mto Igombe unaomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na msitu wa Hifadhi wa Ushetu Ubagwe unaomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Alisema,mgogoro huo umetokana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuweka alama za mipaka kwenye eneo la Hifadhi ya Msitu wa Ushetu Ubagwe uliopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoani Shinyanga.
“ Hata hivyo , kwa mujibu wa Matangazo ya Serikali ya uanzishwaji wa Hifadhi ya Msitu wa Igombe river, Tangazo la Serikali Namba 32 la mwaka 1958 na Hifadhi ya msitu wa Ushetu Ubagwe, Tangazo la Serikali na 442 la mwaka 1958 hakuna mwingiliano wa mipaka kati ya Hifadhi hizi mbili.”alisema Katimba
Alisema,Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) itaendelea kuhakikisha Hifadhi ya Msitu wa Igombe river inabakia kwenye mipaka yake kama ilivyo kwenye Tangazo la Serikali Namba 32 la mwaka 1958 la uanzishwaji wa Hifadhi hiyo.
Katika swali la nyongeza Cherehani alisema mgogoro huo bado upo na kwamba hata kipindi Rais Samia Suluhu Hassan alipoteua Mawaziri wanane waliokwenda shinyanga, mkoa ulitoa taarifa juu ya mgogoro huo.
“Na ilifikia hatua wananchni wagu zaidi ya 17 walikamatwa kimakosa wakiwa na vibali na mali zao zikataifishwa zikapelekwa Kaliua, na kuna kipindi ilifikia hatua kati ya askari wa TFS upande wa Kaliua na askari wa halmashauri ya wilaya ya Ushetu wakakutana kwenye mipaka na baada ya kuona mipaka,hifadhi ya Igombe ikahamishwa kuja eneo la Ushetu ,
“Na Kamishna wa Ardhi aliagizwa na alishafika na timu yake akafanya tathmini ya kusoma na kutafsiri ramani upya na kilichokuwa kimebaki ni Waziri kuja kutangaza tu mipaka ikae wapi, ni lini sasa Waziri wa Ardhi atakuja na kutafsiri na kusoma mipaka ili kuondoa muingiliano uliopo kwa wananchi wake.?”amehoji Cherehani
Akijibu swali hilo,Katimba amekiri kuwepo kwa changamoto ya tafsiri ya mipaka katika hifadhi hizo.
“Kweli kumekuwa na changamoto ya tafsiri ya mipaka katika hifadhi hizo ,lakini hata hivyo dhamana ipo chini ya Wizara ya Ardhi na Waziri tayari analifahamu suala hilo na atalishughjulikia ili kumaliza mgogoro huo.” Amesema Katimba
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Godfrey Pinda amemtaka Mbunge huyo wakutane kwa ajili ya kujenga hoja juu ya suala hilo ambalo tayari limeshafanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa .
More Stories
Samia awataka wanahabari kutanguliza uzalendo mbele
UAE yamtunuku Rais Samia Medali ya juu kabisa
Rais Samia amteua Mkurugenzi Mtendaji TANESCO