May 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge ahoji matumizi holela ya msumeno nyororo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma  

SERIKALI kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Maliasili na Utalii, inatekeleza mpango wa muda mrefu wa Mkakati wa Kurejesha uotonwa asili  kwa kupanda miti maeneo yaliyoharibiwa Takribani Hekta Millioni 5.2 ifikapo 2030. 

Hayo yamesemwa Jana Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Kazi,Ajira na Wenye ulemavu Patrobasi Katambi wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kuhusu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini Profesa  Patrick Ndakidemi.

Katika swali lake Profesa Ndakidemi alitaka kujua ni upi mpango wa Taifa wa kupanda miti kwa kipindi cha muda mfupi na mrefu ili kukabiliana na janga la kukata miti.

Katambi amesema,shughuli zinazoendelea ni pamoja na kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kupitia kampeni za upandaji miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa kila mwaka.

Lakini pia amesema ipo  Kampeni maalumu ya Soma na Mti, ambapo Serikali amewataka wanafunzi wote wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kupanda miti na kuitunza katika kipindi chao chote cha masomo wawapo mashuleni na vyuoni. 

Aidha alisema, Serikali kupitia Wakala wa misitu Tanzania (TFS) imeendelea kuzalisha miche ya miti ya aina mbalimbali na kuigawa bure kwa Wizara na Taasisi, Wadau, Sekta Binafsi pamoja na wananchi kwa lengo la kupanda miti katika maeneo yao kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tunarejesha uoto wa asili nchini.

Ametumia nafasi hiyo  kutoa Rai kwa wananchi na Sekta binafsi kuendelea kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na uharibifu wa ardhi, na kuenea kwa jangwa na ukame. 

Katika maswali yake ya nyongeza Prof.Ndakidemi alitaka kujua Serikali inatoa tamko gani kuhusu uwepo wa majangili  wanaotumia mashine ya  msumeno nyororo kukata miti na kuwa kikwazo kikubwa sana kwa Serikali kwa sababu wanaharibu mazingira ya miti  iliyopandwa na miti ya asili na inayotunza vyanzo vya maji 

 Pia Mubunge hiyo alitaka kujua Serikali ina mipango gani ya kufuatilia na kufanya tathimini ya miradi ya kupanda miti Ili kuangalia kama kuna ufanisi au changamoto katika miradi inayotekekezwa hapa nchini

Akijibu maswali hayo Katambi alisema,zipo taratibu na miongozo ya kufuata katika matumizi ya mashine hizo .

Kufuatia Hali hiyo amepigia marufuku kwa mtu yeyote kutumia mashine hiyo bila kuwa na kibali halali Kutoka Mamlaka zilizopo maeneo husika hasa Halmashauri

Vile vile amesema,zipo timu zinafanya tathimi ya kuhakikisha upandaji miti unafanyika  na iliyoharibika inachukuliwa hatua ya kurejesha Ili kurudisha uotonwa asili.