
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
Serikali imekamilisha usanifu wa daraja la Sanza pamoja na barabara za kuingia na kutoka (approach roads) zenye urefu wa kilomita 14, na tayari mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alitoa taarifa hiyo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dkt. Pius Chaya. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini ujenzi wa daraja hilo utaanza rasmi.
Aidha, Dkt. Chaya pia alitaka kujua ni lini Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) utaanza kuhudumia barabara ya Kintiku–Makanda–Chemba–Kondoa, ambayo kwa sasa iko chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), kufuatia maamuzi ya kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa wa Singida kilichopitisha ombi la kuhamisha barabara hiyo.
Katika swali la msingi, Mbunge huyo alihoji kuhusu lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Manyoni Mashariki – Heka – Sanza – Chali Igongo – Bihawana – Dodoma Mjini kwa kiwango cha lami.
Akijibu, Mhandisi Kasekenya alisema kuwa kazi ya Serikali ni kupokea maombi na kisha kutuma wataalamu kufanya tathmini ili kuona kama barabara inakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi. Ikiwa itakidhi, basi itapandishwa hadhi na kuanza kuhudumiwa na TANROADS.
Kuhusu ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, Mhandisi Kasekenya alisema maandalizi yameanza kwa barabara ya Manyoni Mashariki – Heka – Sanza – Chali Igongo (mpaka wa mikoa ya Singida na Dodoma) – Kipanga – Kidiho – Bihawana Junction yenye urefu wa kilomita 192.
Alifafanua kuwa taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina zinaendelea, na kazi hizo zinatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 2026.
“Baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi,” alisisitiza Mhandisi Kasekenya.
More Stories
AAFP yampitisha Ngombare Mwiru kugombea Urais Bara
DC Mpogolo:DMDP kujenga barabara za urefu km 67 Ilala
Uhakiki na uchambuzi wa kazi za waandishi wa tuzo za Samia Award wafanyika kwa weledi