Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Ilala
Wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Zanaki,wametakiwa kulinda heshima ya shule hiyo na kuwa mabalozi wazuri huko wanapoenda pamoja na kuzingatia elimu waliopata shuleni hapo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati za Uchumi na Huduma za jamii Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam Saady Khimji ambaye ni Diwani wa kata ya Ilala,katika mahafali ya kidato cha sita shule ya sekondari Zanaki wilayani Ilala.

“Nawaomba vijana wangu mkalinde heshima na kutengeza hadhi ya shule yetu iliyopo kata ya Upanga,kwenda kuwa mabalozi wa shule hii mkatangaze mazuri ya Zanaki,”amesema Khimji.
Khimji,amewataka wanafunzi wa shule hiyo wanaojiandaa na mitihani ya taifa,unatarajiwa kuanza Mei 5,2025, wazingatie elimu waliopata shuleni hapo kwani walimu,na wazazi wanatarajia kuona wanafaulu kwa asilimia 100 ili waweze kufikia elimu ya juu.
Aidha aliwataka wahitimu hao wanaokwenda kufanya mitihani yao kumtanguliza Mwenyezi Mungu ili waweze kufanya vizuri na kupata matokeo mazuri ya mitihani yao.
Kwa upande wake Ofisa Elimu,Vifaa na Takwimu wa Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam,Liberia Minja, amewataka wahitimu wazingatie yote waliolelekezwa na kuyafanyia kazi kwakuwa kidato cha sita sio mwisho wa elimu hivyo wasibwete wakasome kwa bidii watengeneze CV zao.
Mkuu wa shule ya sekondari Zanaki,Delvine Koka, amesema matarajio ya shule hiyo kwa wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu,watafaulu kwa asilimia 100 kutokana na kuandaliwa vizuri na walimu.

“Shule yetu inafanya vizuri kwa miaka mitatu mfululizo, hakuna daraja sifuri idadi kubwa ya wanafunzi wanapata daraja la kwanza mpaka la tatu ni miongoni mwa shule za mjini zinazopata tuzo,”amesema Delvine.
More Stories
CCM yalaani shambulio dhidi ya Padre Kitima
Kibasila wafurahia mafanikio ufaulu asilimia 100 kwa miaka mitatu
DAS Ilala awafunda wahitimu Benjamin Mkapa