May 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandikishaji wapiga kura watakiwa kuzingatia weledi

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online Nkasi

Maofisa waandikishaji wasaidizi na waendesha vifaa wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kufanikisha jukumu hilo muhimu la kitaifa.

Wito huo umetolewa na Oisa Mwandikishaji wa Wilaya ya Nkasi, Ladislaus Mzelela, wakati akifunga mafunzo ya siku moja kwa maofisa hao.Ambapo amesisitiza kuwa jukumu hilo ni kubwa na linahitaji uelewa wa kina, weledi na uzingatiaji wa maadili ya kazi ili kuhakikisha kila mwenye sifa anapata haki ya kuandikishwa.

“Uweledi pekee ndio utakaopelekea kazi hii kufanyika kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria,”amesema.

Mzelela,pia amewataka maofisa hao kutambua uzito wa kazi waliyopewa kwani wao ndio wawakilishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi vituoni.Hivyo ameonya kuwa ukiukwaji wa maadili au kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu kunaweza kuleta athari kwa taifa zima.

Kwa upande wake,Ofisa Uchaguzi wa Wilaya ya Nkasi, Atufigwege Mwakitega,amewataka waandikishaji kuhakikisha wanatunza kwa uangalifu vifaa vyote vya kazi watakavyokabidhiwa, kwani ufanisi wa kazi yao unategemea utunzaji mzuri wa vifaa hivyo.

Amewakumbusha kuwa tabia njema na kuepuka vitendo vya ulevi ni muhimu wakati wote wa siku saba za utekelezaji wa zoezi hilo litakaloanza rasmi Mei 1, 2025.

Mafunzo hayo yalijumuisha somo la ujazaji wa fomu mbalimbali zinazohusiana na zoezi hilo, zikiwemo fomu za kiapo cha kutunza siri, kujitoa uanachama wa chama cha siasa, na utaratibu wa kuwaandikisha wapiga kura wapya au wanaofanyiwa marekebisho kwenye taarifa zao.