April 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia :Kadiri nchi inavyofunguka ndivyo inavyohitaji mabadiliko ya sheria

Na Penina Malundo,Timesmajira 

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kadiri nchi inavyofunguka na kuendelea, ndivyo inavyohitaji mabadiliko ya sheria ili kulinda maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia amesema uzinduzi wa toleo jipya la juzuu za sheria zilizofanyiwa marekebisho ni hatua muhimu katika kupambana na matumizi mabaya ya madaraka na kuongeza uwazi katika utawala wa sheria nchini.

Akizungumza leo Ikulu jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa sheria hizo, Rais Samia alisema kuwa kuanzia mwaka 2002 hadi 2023 jumla ya marekebisho 1,039 ya sheria mbalimbali yamefanyika. 

Amesema idadi hiyo inaonesha jinsi nchi inavyofunguka na hivyo kuhitaji sheria zinazokwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Rais Samia amesema kuwa uhuishaji wa sheria haupaswi kuwa tukio la kila baada ya miongo miwili bali kila baada ya miaka 10. Aidha, ameeleza kuwa ndani ya kipindi hicho cha miaka 10, sheria zinapobadilika zinapaswa kuandikwa na kuingizwa katika mpango wa marekebisho ya kila mwaka, na baadaye kuunganishwa kutengeneza juzuu.

” Serikali itaendelea kuwekeza katika urekebishaji wa sheria ili ziendane na mahitaji ya wakati ambapo urekebu mwingine wa sheria umepangwa kufanyika mwaka 2033.

“Sheria hizo zilizoboreshwa zitaziba mianya ya kisheria ambayo hapo awali ilitumiwa na baadhi ya watu kwa manufaa binafsi, ikiwa ni pamoja na kuchochea vitendo vya rushwa,”amesema.

Aidha amesema uzinduzi wa toleo jipya la juzuu za sheria zilizofanyiwa marekebisho ni hatua muhimu katika kupambana na matumizi mabaya ya madaraka na kuongeza uwazi katika utawala wa sheria nchini.

“Ile ‘tazama kule, tazama kule’ ya kisheria ili mtu apenyeze yake sasa hakuna. Sheria zimeandikwa upya, zimepangwa vizuri, ziko wazi, zinapatikana kwa urahisi na zinaeleweka kwa wananchi. Hii itapunguza uwezekano wa watu kutenda makosa kwa kisingizio cha kutojua sheria,” amesema Rais Samia.

Amesema kuwa msingi mkuu wa Serikali ni sheria, na bila sheria, hakuna kinachoitwa Serikali.

 Rais Samia alinukuu kauli ya Baba wa Taifa “Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema, Serikali ni sheria. Hakuna Serikali bila sheria. Na sheria zikishaundwa, ni lazima zifuatwe,” amesema Rais Samia.

Amesema sheria zilizofanyiwa marekebisho si tu nyenzo ya kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, bali ni msingi imara wa kujenga Taifa linalozingatia haki, amani na maendeleo.

“Waheshimiwa viongozi na wananchi wenzangu, ninapoelekea kuhitimisha niseme kuwa toleo la sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebishaji ni dhamira ya dhati ya Serikali kujenga Taifa linalosimamia utawala bora na wa sheria kwa kuwa na sheria zilizowekwa wazi, zilizo sahihi na zinazoeleweka,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha kutekelezeka kwa mradi wa Urekebu wa sheria Toleo la mwaka 2023.

Amesema kuwa hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mradi huo kufanyika kwa rasilimali za ndani ya nchi zikiwemo fedha za makusanyo ya ndani na watumishi.

Amesema jambo hilo ni hatua ya kihistoria iliyofanikishwa chini ya Serikali ya awamu ya sita, kwani ni tofauti na Toleo la mwaka 2002 ambalo lilifadhiriwa na Benki ya Dunia na kwamba hiyo inaashiria dhamira ya kweli ya Taifa la Tanzania kujitegemea na kuwekeza katika mifumo imara ya kisheria kwa maendeleo ya Taifa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa urekebu uliofanyika ni kazi ya msingi ambayo inakwenda kuhuisha, kuboresha na kurahisisha matumizi ya sheria za nchi na kwamba kwa kufanya hivyo kutahakikisha kuwa sheria za nchi zitabaki kuwa hai, zinazoendana na wakati na kueleweka na wananchi wote.

Amesema zoezi la urekebu sasa litaweza kufanyika kila baada ya miaka kumi,ambapo watahakikisha sheria zinabaki kuwa hai, zinazoendana na wakati na zinaeleweka kwa urahisi na wananchi wote.

” Zoezi hili limehusisha kusasisha (update) sheria zote kwa kujumuisha marekebisho yaliyofanyika tangu Toleo la mwisho mwaka 2002, kurekebisha makosa ya kiuchapaji na kuziweka sheria hizo katika mfumo unaoeleweka.

“Toleo la Urekebu utakalozindua leo linajumuisha Sheria Kuu (Principal Legislation) 446 ambazo zimegawanywa katika Juzuu 21, ikiwemo Fahirisi (index),hivyo miongoni mwa hizo ni pamoja na Sheria mpya 171 zilizotungwa kati ya mwaka 2002 na 2023,”amesema

Amesema toleo hili ni zao la kazi ya miaka minne (2020 – 2024) na limefanikishwa kwa kutumia rasilimali za ndani pekee chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Toleo hilo la sheria zilizorekebishwa litaanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2025, na linatajwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya kisheria yanayoendelea nchini.

Na toleo hilo linajumuisha sheria kuu 446 ambazo zimegawanywa katika Juzuu 21 ikiwemo farihisi, ambapo miongoni mwa hizo ni pamoja na sheria mpya 171 zilizotungwa kati ya mwaka 2003 hadi 2023.