Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
NDANI ya kipindi kifupi cha miezi minne tangu kuzinduliwa kwake, Mfuko wa iCash unaosimamiwa na iTrust Finance umeonesha mafanikio makubwa kwa kuongezeka kwa asilimia 49.85 ya thamani yake, na hivyo kuwa miongoni mwa njia salama zaidi za uwekezaji nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na kampuni ya iTrust Finance Limited, Mfuko huu uliozinduliwa rasmi tarehe 3 Desemba 2024 na ulianza kwa mafanikio makubwa, ambapo TZS bilioni 12.79 zilikusanywa kupitia mauzo ya awali ya hisa—ikiwa ni ongezeko la zaidi asilimia 28 ya matarajio.
Miezi mitatu baadaye tarehe 31 Machi 2025, thamani ya mfuko huu ilikuwa imefikia TZS bilioni 19.18, huku ikirekodi faida ya asilimia 3.57 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.
iCash ni mfuko wa soko la fedha uliobuniwa kwa ajili ya wawekezaji wanaotaka faida ya muda mfupi zaidi yenye uwezekano mdogo wa kuingia hasra. Hii ni kutokana na uwekezaji wa fedha za mfuko huu katika hati fungani mbalimbali za serikali ambapo jumla ni asilimia 69.2% ziliwekezwa, huku hati fungani za makampuni binafsi zikiwa ni asilimia 29.4% na fedha taslimu zikiwa ni asilimia 0.8%. Huu ni uwekezaji unaolinda mtaji wa mwekezaji huku ukitoa faida ya kiasi bila hatari kubwa.
Aidha mfuko wa iCash hauna ada ya kujiunga wala ya kujitoa, na pesa za mwekezaji zinaweza kurejeshwa ndani ya siku tatu za kazi. Hivyo, ni chaguo linalotoa uhuru na thamani kwa mwekezaji wa kawaida.
“Mfuko wa iCash umepokelewa vizuri na wawekezaji wanaotaka faida ya uhakika na isiyo na msukosuko,” alisema Faiz Arab, Mkurugenzi Mtendaji wa iTrust Finance. “Utendaji wake mzuri unathibitisha dhamira yetu ya kutoa mfuko wa kuaminika unaosimamiwa kitaalamu kulingana na hali ya soko ya sasa.” aliongezza
Mafanikio ya mfuko huu yamekuja wakati ambapo soko la hati fungani za serikali linaendelea kufanya vizuri. Mwezi Machi pekee, serikali ilifanya minada miwili ya hati fungani na kukusanya jumla ya TZS bilioni 661.59, ikivuka matarajio kwa viwango vya riba vya wastani vya asilimia 10.75 na 9.48. Hali hii imenufaisha sana mifuko ya muda mfupi kama iCash, ambao huendana kwa karibu na viwango vya hati fungani za serikali za siku 364.
Mfuko wa iCash unasimamiwa na kusajiliwa chini ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), jambo linalohakikisha usalama na uangalizi wa maslahi ya wawekezaji.
Kwa kuanzia na uwekezaji wa chini wa TZS 100,000 na nyongeza ya uwekezaji kuanzia TZS 10,000 tu, iCash umefungua milango kwa Watanzania wengi kuanza safari yao ya uwekezaji kwa njia rahisi na salama.
Kadri Watanzania wanavyozidi kuelewa umuhimu wa kujiwekea akiba na kuwekeza kwa mpangilio, iCash inajitokeza kama njia bora, salama na ya kuaminika ya kukuza fedha kwa uangalifu.
More Stories
Dkt.Biteko:Wazazi msiwahusishe watoto kwenye migogoro yenu
Waziri Lukuvi amuwakilisha Rais Samia Tabora
Thabo Mbeki aipongeza Tanzania kuandaa mhadhara wa UNISA mara tatu mfululizo