May 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yatuma salam za pole kifo cha Baba Mtakatifu Francisko

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIKA hali ya majonzi na huzuni kuu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa salamu za pole na rambirambi kwa waumini wa Kanisa Katoliki pamoja na jamii ya kimataifa kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Francis, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, kilichotokea mapema siku ya Jumatatu.

Kupitia taarifa yake kwa umma, CCM imesisitiza kuwa kifo hiki ni pigo kubwa si tu kwa Wakristo wa Kanisa Katoliki, bali pia kwa watu wote walioguswa na ujumbe wa amani, mshikamano na upendo alioueneza Papa Francis kwa kipindi chote cha uongozi wake wa kiroho.

Chama kimeeleza kuwa kinatambua na kuheshimu mchango wa Baba Mtakatifu kama kiongozi wa kipekee aliyekuwa mstari wa mbele katika kutetea utu wa mwanadamu bila ubaguzi wa dini, rangi wala utaifa. Kwa moyo wa huruma na msimamo thabiti, alisimamia haki na usawa na alisisitiza mazungumzo kati ya dini mbalimbali, jambo lililojenga misingi ya amani ya kudumu duniani.

Kwa namna ya pekee, CCM imetoa pole kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ikiwaombea faraja, subira na nguvu wakati huu wa majonzi na maombolezo makubwa. Pia, imesisitiza kuwa ujumbe wa matumaini alioueneza Papa Francis utaendelea kuishi katika mioyo ya watu wote waliompenda na kuongozwa naye.

Kwa niaba ya wanachama wake na Watanzania kwa ujumla, CCM imetoa sala na maombi kwa Mwenyezi Mungu ili aipokee roho ya Baba Mtakatifu na kuilaza mahali pema peponi.

Baba Mtakatifu Francis atakumbukwa milele kama sauti ya haki, matumaini na mwanga wa amani kwa dunia nzima.