April 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini watoa wito tunu za taifa kuheshimiwa

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

Viongozi wa dini mkoani Mwanza wametoa wito kwa Watanzania wote, hususani wanasiasa na vyombo vya dola, kuheshimu na kuenzi tunu za taifa ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Wito huo umetolewa katika kongamano la amani lililowakutanisha viongozi wa dini, wanasiasa, vyombo vya ulinzi na usalama, waendesha bodaboda na machinga.

Tunu saba zilizosisitizwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na matumizi ya lugha ya taifa. Kwa mujibu wa viongozi hao, utekelezaji wa tunu hizo kwa vitendo ni msingi wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, usawa na bila migogoro ya kisiasa.

Sheikh Hassan Kabeke, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza,ameeleza kuwa matumizi ya lugha chafu, matusi, na upendeleo kutoka kwa vyombo vya dola ni mambo yanayoweza kuchochea machafuko.ameonya kuwa siasa siyo mchezo wa kudhalilisha bali ni njia ya kuwahudumia watu kwa heshima na utu.

“Mwanasiasa anapotoa lugha za kudhalilisha, hata kwa wafu, anakiuka tunu ya utu. Rushwa na matumizi mabaya ya vyombo vya dola ni hatari kwa uadilifu wa uchaguzi.Tume Huru ya Uchaguzi ihakikishe uwazi na kutotumiwa kuvuruga uchaguzi,”.

Aidha,amekemea matumizi ya vijana kwa ajili ya kuchochea vurugu, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa kudai haki katika jamii.

Kwa upande wake, Askofu Dkt. Charles Sekelwa, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, amesisitiza kuwa ukosefu wa uwazi, ushirikishwaji na uadilifu ni kiini cha migogoro mingi ya kijamii na kisiasa.

Hivyo amewataka viongozi wa taasisi, serikali na dini kuonesha mfano wa utiifu kwa Katiba na maandiko ya kidini kama njia ya kulinda tunu za taifa.

“Kiongozi asiye mzalendo ni tishio kwa taifa. Mzalendo wa kweli yupo tayari kulinda nchi yake, dini yake, taasisi yake na jamii yake kwa gharama yoyote.Ni muhimu kwa viongozi wa serikali kufuata sheria na katiba ya nchi,”amesema Askofu Sekelwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Changu Ng’oma,amehimiza wapiga kura kutokubali kushawishiwa na propaganda au ahadi zisizotekelezeka.Hivyo wananchi wanapaswa kuwauliza wagombea maswali magumu kabla ya kuwapa dhamana ya uongozi.

“Elimu kuhusu tunu za taifa ni muhimu ishuke hadi ngazi ya familia,tusiuze utu wetu kwa fedha au ahadi hewa,”amesema Ng’oma.

Naye Mchunguzi Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Nyamagana, Protasi Andrew,amewataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa, akisisitiza kuwa rushwa ni tishio kwa uongozi bora na maendeleo ya taifa.