Na Judith Ferdinand
Kayenze ni moja ya kata 19 zinazounda wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, iliopo kandokando ya Ziwa Victoria na shughuli kubwa ya kiuchumi inayowashughulisha wakazi wake ni uvuvi.
Mbali na uvuvi, pia zipo shughuli nyingine zinazofanyika kwa ajili ya watu kujiingizia kipato, ikiwemo mama lishe, wachuuzi wa samaki, usafiri na vitu vingine vingi ili mradi kila mtu anahangaika mkono uende kinywani
.
Ni Machi 17, 2025, majira ya asubuhi nikiwa eneo la kupumzikia abiria wanaosubiri kivuko (ferry) cha Mv. Ilemela katika gati la Kayenze, kwenda kisiwa cha Bezi kilichopo wilayani Ilemela.

Shughuli mbalimbali zinaendelea huku wauzaji wa bidhaa mbalimbali wakiendelea kunadi biashara zao, mara nasikia sauti ya kike ikinadi biashara yake ya karanga, kuinua kichwa nakutana na binti ambaye kwa kumtazama umri wake ni chini ya miaka 20, akiwa amebeba ndoo ndogo yenye karanga za kuchemsha huku akiwa na mtoto mgongoni. Ninajiuliza maswali ambayo majibu yake anayo binti huyo.
Ninamuita kisha tunafanya mazungumzo. Kwanza ananielezea historia yake. Huyu si mwingine bali ni Kokusima Mukama (siyo jina lake halisi), mama wa watoto wawili ambaye ameolewa na mmoja wa wavuvi katika kata hiyo.
Maisha ya Kokusima
Simulizi ya binti huyu mwenye umri wa miaka 22 ni ndefu. Akiwa ni mtoto wa nne kati ya watoto wanane kwa mama yake, alizaliwa kata ya Lutare na kuishi na wazazi wake, lakini katika kukua kwake alijikuta anakatisha masomo akiwa darasa la pili baada ya baba yake mzazi ambaye alikuwa mvuvi kuitelekeza familia na kumuachia mama yao majukumu ya malezi peke yake.
Anasimulia kuwa kutelekezwa kwa familia kulichangia malezi duni pamoja na kuleta ugumu wa wao kupata mahitaji muhimu, achilia mbali kupata fursa ya kuendelea na shule.
Hata hivyo, anaeleza kuwa maisha yake ya shule hayakuwa mazuri kutokana na mama yake kushindwa kuhudumia familia yenye watoto wanane peke yake kwani hakuwa na shughuli maalumu ya kumuingizia kipato cha kutosheleza mahitaji ya kawaida ya familia.
“Mama alishindwa kugawanya kipato kwa ajili ya mahitaji ya shule na chakula nyumbani, kuna wakati ilitulazimu kunywa uji ndio tulale, na wakati mwingine tulilala njaa. Hivyo huwezi kwenda shule ukiwa na njaa bora ubaki nyumbani,” anasimulia.
Anaeleza kuwa kutokana na mazingira hayo, aliamua kuacha shule, lakini aliendelea kukaa nyumbani huku akiendelea kushuhudia ugumu wa maisha wanayopitia kama familia, huku mama akihangaika kuhakikisha wanapata walau chakula.
Mazingira yaliyosababisha Kokusima kukatisha masomo akiwa darasa la pili, yalisababisha akose haki ya msingi ya kuendelezwa ambayo inahusu maendeleo ya mtoto kiakili ikijumuisha elimu rasmi na isiyo rasmi, tamaduni, mila na desturi sahihi za jamii yake, kiroho kwa maana ya imani na vipaji.
Haki hizo ni pamoja na nyingine za watoto zinazolindwa katika mikataba mikubwa miwili ya haki za watoto, ambayo ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990.
Tanzania imeridhia mikataba hiyo miwili ambayo inatoa wajibu kwa serikali, wazazi, walezi na wanajamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na ubaguzi.
Katika kuwezesha utekelezaji wake Tanzania imetunga Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo inataja haki zote za msingi za mtoto kama zilivyoelezwa kwenye mikataba hiyo.
Pia sheria hiyo imeweka bayana kwamba uamuzi wowote kuhusu mtoto lazima uzingatie maslahi yake kama yanavyotajwa kwenye sheria na kanuni zake.
Kokusima angeliweza kupata haki yake ya elimu kama mamlaka zingesimamia Sheria ya Elimu Namba 25 ya 1978 na maboresho mwaka 2016, ambayo inalinda haki ya mtoto ya kupatiwa elimu, ikieleza wazi kwamba elimu ya msingi ni ya lazima kwa watoto wote na itatolewa bure.
Kadhalika, kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo zinaweka bayana kwamba ni kosa kwa mzazi kushindwa kumwandikisha shule mtoto mwenye umri wa kwenda shule, pia ni kosa kwa mzazi anayeshindwa kumsimamia mtoto wake mpaka kuhitimu darasa la saba.
Kwa mujibu wa sheria hiyo na kanuni zake, utoro ni kosa la jinai na hivyo mtoto mtoro au mzazi ambaye anasababisha mtoto wake awe mtoro wote wanaweza kushitakiwa kwa kosa la jinai.
KUOLEWA NA KUISHI NA MME
Kokusima anaeleza kuwa kuacha shule hakukumsaidia yeye na familia yake kupata unafuu wa maisha, kwani ugumu wa maisha ulibaki palepale kutokana na kumtegemea mama peke yake kusimamia familia bila msaada wa baba.
Anasema baada ya mama yake kufariki mwaka 2019, hali ilizidi kuwa ngumu. Mwaka huo huo katika harakati za kuhangaika namna ya kujikomboa kutoka katika hali duni alikutana na mwanaume ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 32 anayejishughulisha na uvuvi, akamshawishi kuingia katika ndoa akiwa na umri wa miaka 15 tu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto namba 21 ya 2009, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto pamoja na Sera ya Maendeleo ya Mtoto, mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18.
Utafiti wa Shirika la World Vision Tanzania wa hivi karibuni unaonyesha kuwa takribani asilimia 31 ya watoto wa kike wameolewa wakiwa na umri chini ya huo.
“Hii ni idadi kubwa na inapaswa kukomeshwa ili watoto wa kike walindwe na kuendelea sawa na watoto wa kiume, ndoa za utotoni zinavunja haki za binadamu ambazo zinaelekeza kuwa mtu ni lazima awe na umri wa mtu mzima pale anapoingia katika ndoa, kwa ridhaa yake,” inasomeka sehemu ya chapisho la taasisi hiyo.
Takwimu za Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (TDHS), 2015-2016 zinaonyesha kuwa asilimia 36 ya mabinti wenye miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Adha kwa mujibu wa TDHS mwaka 2016 mikoa yenye viwango vikubwa vya ndoa za utotoni nchini ni pamoja na Shinyanga asilimia 59, Tabora asilimia 58, Mara asilimia 55 na Dodoma asilimia 51.
Kwa mujibu wa wataalamu, viwango hivyo ni sawa na kusema kuwa kwa wastani, wasichana wawili kati ya watano huolewa kabla hawajatimiza umri wa miaka 18.
Kokusima anaeleza: “Baada ya kuolewa nilikaa takribani miaka miwili nikapata ujauzito nikiwa na miaka 17 na kufanikiwa kujifungua mtoto wangu wa kwanza wa kiume ambaye sasa ana miaka mitatu na miezi 11 baada ya hapo nilikaa takribani miaka miwili tena nikabeba mimba ya mtoto wangu wa pili wa kike ambaye sasa ana miezi 11, na ndiye ninayetembea naye mgongoni wakati wa kufanya biashara.”
Anasema sababu ya kukubali kuolewa katika umri huo, aliamini kuwa atapata unafuu wa maisha hali ambayo imekuwa tofauti kidogo na matarajio yake.
“Maisha ni magumu ingawa unafuu upo kwa kiasi kidogo, ninalazimika kufanya biashara ya karanga nikiwa na mtoto mgongoni ili kusaidia kipato na majukumu mume wangu, kutokana na shughuli yake ya uvuvi siyo kila siku anaweza kupata samaki wakati mwingine anakosa,” anasema Kokusima.
Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa wanawake wanaoishi katika kaya maskini asilimia 46, wana uwezekano mkubwa mara tatu zaidi kuolewa kwa mara ya kwanza wakiwa bado watoto kuliko wanaoishi katika kaya tajiri ambao ni aslimia 16.
MAISHA YA NDOA
Kokusima anasema maisha ya ndoa si rahisi kama vile watu wanavyodhania, yanahitaji uvumilivu hasa kwa mabinti waliolewa wakiwa na umri mdogo.
Kutokana na shughuli anayofanya mume wake kuna muda samaki ziwani zinakuwa za shida, hivyo kumpa wakati mgumu yeye kuhudumia familia kutokana na kuuza karanga tu.
“Tukipata tunakula, wakati mwingine tukikosa tunalala njaa ila tunahakikisha watoto hawakosi chakula. Tunahangaika katika kutafuta fedha kwani kwenye uvuvi huwezi kutegemea, kuna kupata samaki na muda mwingine kukosa, muda mwingine unasema ukae tu ndani inakuwa shida.
“Natoka nyumbani saa mbili au tatu asubuhi, naanza kutembeza karanga kwa ajili ya kutafuta wateja katika eneo hili la Kayenze Centre, hasa nikitega watu wanaosafiri kwenda Bezi au Ukerewe. Wakati mwingine nikiwa na mzigo mwingi nalazimika kuvuka maji hadi kisiwani Bezi kwa ajili ya kupeleka biashara, huku nikiwa nimembeba mtoto wangu mdogo mgongoni na mwingine namuacha na baba yake, kwani muda huo anakuwepo nyumbani maana yeye hufanya shughuli usiku,” anasimulia.
Hata hivyo, anaeleza kuwa akiwa eneo la Kayenze Centre analazimika ikifika saa sita kurudi nyumbani kwa ajili ya kupika chakula cha familia, majira ya saa tisa alsiri anarejea kwa ajili ya kumalizia biashara kwa kutegeshea abiria wanaotoka Ukerewe au kisiwa cha Bezi. Saa 11 jioni anafuata mzigo kwa ajili ya kesho na kurejea nyumbani.
“Changamoto kwenye ndoa zipo hasa tulio olewa katika umri mdogo, baba asingetelekeza familia na baadaye mama yangu kufariki, hakika ningetimiza ndoto yangu ya kuwa mwalimu na wala nisingeolewa katika umri huo,” anasisitiza.
NINI ILIKUWA NDOTO YAKE
Kokusima anasema laiti angefanikiwa kusoma na kufikia ngazi ya chuo, alitamani kuwa mwalimu ndoto ambayo anaeleza kuwa haikufanikiwa kwa sababu ya baba kutelekeza familia hivyo kuwa kama alivyo sasa.
Hata hivyo, anasema kwa sasa hatamani tena kusoma hata kama angetokea mtu wa kumsomesha, kwani anajikita zaidi kuhudumia watoto wake na kuhakikisha kuwa hawatakosa fursa ya kupata elimu na kufikia ndoto zao.
“Sasa nimekuwa mwalimu mzuri kwa mabinti wenzangu, kwa uwezo wa Mungu nitahakikisha watoto wangu wa kike hawaingii kwenye ndoa za utotoni. Kwa sasa maisha ya kusoma hapana, muda umeishapita sana, labda kupata mafunzo ya ujuzi mbalimbali,” anasema.
WITO KWA MABINTI, WAZAZI NA SERIKALI
Kokusima anaeleza kuwa pamoja na kwamba yeye alikwama kimasomo, lakini wasichana wanapaswa kuzingatia masomo na kujiepusha na vishawishi ili kutimiza ndoto zao hata kama hali ya uchumi wa familia ikiwa duni.
“Nilikuwa na ndoto za kuwa mwalimu, lakini nimeangukia katika ndoa na mimba za utotoni, kulea mtoto kuna changamoto kwa sababu umri wangu ulikuwa mdogo na hali ya uchumi ilikuwa ngumu,” anasema Kokusima na kuongeza:
“Mabinti wenzangu ambao wazazi wao wanajiweza au kupata fursa wasome kwani kuolewa mapema hakuna kitu ambacho wanaweza kupata na badala yake wanashindwa kutimiza ndoto zao na kuwa tegemezi.”
Amewataka wazazi kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ya msingi kwa watoto ili kuwasaidia wasiingie katika ndoa za utotoni au kufanya shughuli nyingine ambazo zitaathiri ukuaji wao na kukwamisha ndoto zao.
“Wazazi hata wakitengana watimize wajibu wao, kwani ugomvi wao hauwahusu watoto ambao wamekuwa waathirika kwa vitu ambavyo hawajavisababisha. Binti kuingia kwenye ndoa katika umri mdogo kunadhoofisha nguvu kazi ya taifa na kufanya kuwa na kizazi ambacho wanawake wake hawajaenda shule,” anafafanua.
Anatoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kufanya jitihada za ziada ili kuhakikisha ndoa za utotoni zinakomeshwa, hali itakayotoa fursa kwa watoto wa kike kusoma na kutimiza ndoto zao.
Anataka juhudi za kutokomeza ndoa za utotoni zipewe kipaumbele zaidi ili kusaidia kupunguza wimbi la taifa kuwa na wanawake wengi, lakini tegemezi au wasiopata fursa katika kazi zinazohitaji elimu.
Akiwasilisha mada katika mafunzo kwa waandishi wa habari 31, kuhusu ndoa za utotoni chini ya mradi wa ‘Hapana Marefu Yasiyokuwa na Mwisho’ unaotekelezwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ofisa Ustawi Mkoa wa Mwanza, Baraka Makona, anasema serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kwa ajili ya kutokomeza ndoa za utotoni.
Miongoni mwake ni kusajili na kushirikiana na mashirika yasio ya kiserikali pamoja na taasisi za dini na wadau wengine katika kufanya utafiti, utoaji wa huduma na ufadhili wa shughuli mbalimbali katika kuondokana na ndoa na mimba za utotoni.
Hata hivyo, Kokusima ameiomba serikali ijenge mazingira rafiki kwa watoto wa kike kutimiza ndoto zao na kuepuka kuingia kwenye ndoa za utotoni. Pamoja na kuchukua hatua kuziba mianya yote ambayo inaweza kuchangia mtoto wa kike kupata vishawishi vitakavyofanya binti kuingia kwenye mapenzi akiwa na umri mdogo.
Kadhalika, Kokusima anaungana na wale ambao wamekuwa wakitoa wito kwa serikali kuufanyia kazi mkanganyiko wa kisheria hasa unaogusa umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike.
Sheria ya Ndoa, Sura ya 29 ya mwaka 1971 kama ilivyorekebishwa mwaka 2019, ndiyo inayosimamia masuala ya ndoa nchini Tanzania ambayo inatajwa kuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuruhusu mazingira fulani ya ubaguzi wa kijinsia kwa wanawake na wasichana.
Tamko lililotolewa na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia linasema kuna ukinzani wa kisheria baina ya Sheria ya Mtoto na Sheria ya Ndoa.
Wakati Sheria ya Mtoto ikimtafsiri mtoto kama mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18, Sheria ya Ndoa inaruhusu msichana chini ya umri wa miaka 18 kuolewa na kwa misingi hiyo,sheria inatoa mwanya kwa ndoa za utotoni.
Katika tamko hilo, wanaharakati wanaitaka serikali kutekeleza hukumu ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania iliyothibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ambavyo vinaruhusu mtoto kuolewa na umri wa miaka 15 kwa idhini ya wazazi na 14 kwa ruhusa ya mahakama, kuwa ni vya kibaguzi dhidi ya mtoto wa kike na ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika kesi hiyo ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama ya Rufani ilisema vifungu husika vinapaswa kurekebishwa ndani ya miezi 12 jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika.
Mara kwa mara Serikali imekua ikikiri kwamba kushindwa kubadili kifungu hicho ni kutokana na unyeti wa kitamaduni na wa kidini juu ya jambo hilo. Miaka ya hivi karibuni Jaji Mstaafu Robert Makaramba wa Mahakamu Kuu ya Tanzania, alisema baada ya hukumu ya Mahakama ya Rufani katika kesi hiyo, umri wa kuolewa hauwezi kushushwa na taasisi yoyote ile.
“Hata kama Sheria ya Ndoa haijabadilishwa, lakini katika muktadha wa mamlaka ya mahakama, uamuzi wa Mahakama ya Rufani ni sheria tayari. Bunge linaweza kurekebisha mambo mengine katika sheria husika, lakini suala la umri ambalo limetolewa uamuzi na Mahakama ya Juu kabisa katika nchi yetu, haliwezi kubadilishwa nje ya mfumo wa kimahakama,” alisema Jaji Makaramba katika hafla ya uzinduzi wa machapisho ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).

More Stories
Nchi za Afrika zinavyosisitiza utekelezaji wa SDGs katika kuleta maendeleo Afrika
Umuhimu wa kujadili mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya watoto
Mo Dewji na Urithi anaoujenga ,unavyoenda mbali zaidi ya mafanikio binafsi