April 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wananchi 300 wafanyiwa upasuaji wa macho Mbeya

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

ZAIDI ya wananchi 300 kutoka Mikoa ya nyanda za juu wamefanyiwa upasuaji wa macho katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na wengine 4,000 waliokuwa na uoni hafifu kupatiwa miwani  huku wengine wakipatiwa Rufaa ya matibabu hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwemo watoto wadogo.

Wananchi hao wamefanyiwa upasuaji huo wa macho wakati wengine wakipatiwa  miwani baada ya kupata vipimo kutoka kwa  madaktari bingwa  wa  macho The Bilali Muslim Mission Tanzania kwa uratibu wa Taasisi ya Tulia Trust kupitia wadau mbalimbali.

Kambi hiyo imedumu kwa siku nne kuanzia Aprili 18 mpaka 21 mwaka huu katika viwanja vya shule ya msingi Kagera Kata ya Ilomba.

Akizungumza wakati wa kufunga zoezi hilo  jana April 21,2025,Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini,Rais Umoja wa Mabunge Duniani(IPU),Dkt.Tulia Ackson amesema wananchi waliofanyiwa upasuaji na wamelazwa katika Hosptali ya Rufaa Kanda kwa matibabu zaidi ambapo wengine wanaendelea kuruhusiwa.

Amesema katika kambi hiyo wananchi 4,000 walifanyiwa vipimo vya uchunguzi wa macho na kupatiwa miwani na kwamba wenye changamoto zaidi wamehamishiwa katika Hosptali ya Taifa Muhimbili(Moi).

“Hivyo nitoe  shukrani za kipekee kwa kuja kuungana na kurejesha  tabasamu  kwa watanzania sasa ndugu zangu mmesikia kule Hospitali ya Rufaa Kanda kuna wagonjwa wachache hawa ndugu zetu wataondoka nao mmoja ni  mtoto hali yake sio nzuri ya jicho wataondoka nae  kupata matibabu  katika hospitali ya Taifa Muhimbili,” amesema

Hata hivyo Dkt.Tulia amesema kuwa ili huduma hiyo  iwe imekamilika lazima vifaa viwepo na watalaamu wa kutosha na kusema kuwa hospitali imejitosheleza kwa vifaa kwa ajili ya upasuaji

Aidha Dkt.Tulia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa hospitali Rufaa kanda ya Mbeya kwa upande wa Macho inajitoshereza kwa kuwa na vifaa vya kutosha vya upasuaji wa macho tunashukuru kwa kuendelea kuboresha miundo ya afya kwa hospitali ya Rufaa kanda ambayo inahudumia
Mikoa ya Nyanda za juu kusini.

Kwa upande wake Mratibu wa kambi ya matibabu ya Macho ya The Bilali Muslim mission Tanzania ,Ain Sharif amesema Taasisi ya Tulia Trust wamekuwa na nidhamu ya hali yap juu katika kushirikiana katika kuwajali wananchi katikap siku zote za kutoa huduma kwa wananchi.

Sharif amesema kuwa walijipanga kufanya kazi kubwa kwani mikoa ya nyanda za juu kusini kuna watu wenye matatizo ya macho ikiwemo mtoto wa  jicho ,trakoma,pia kuna watoto wenye matatizo ya macho  na kusema watoto wadogo wanatalkiwa kupewa huduma kwa ngazi maalum lakini pia wamepata mgonjwa ambaye ni mtoto Mdogo wa miaka miwili kutoka mkoa wa Rukwa ambaye wataondoka nae ili akatibiwe hospitali ya Taifa Muhimbili.

Aidha Mratibu huyo ametoa wito wananchi kwenda kupata matibabu hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya kwani tayari wana madaktari bingwa wazuri na manesi na vifaa vya kutosha kwenye matibabu ya macho ikiwemo upasuaji.

Anna kapandila  kutoka Mkoa wa Rukwa  amesema kuwa alitoka  kijijini kwao kuja hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya kupata matibabu ya mtoto wake wa miaka miwili aitwaye Oscar salehe  ambaye ana kansa ya jicho lakini ilishindikana na hivyo kulazimika  na kupewa Rufaa kwenda mkoa wa Kilimanjaro

Nilianzia mkoa wa Rukwa niliposhindwa nikaja hospitali Rufaa kanda ya Mbeya lakini bado ilishindikana tukapewa Rufaa kwenye Moshi nikashindwa kutokana na ukosefu wa fedha ,nikasikia kuna wazungu hapa ikabidi nije wakampima na hivi tunaondoka nao ili wamsaidie mtoto kupata matibabu.