Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
VYOMBO vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya vimetakiwa kuendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na Wadau wengine katika kushughulikia malalamiko na changamoto za huduma za kifedha ikiwemo utapeli na wizi kwa njia ya mtandao.
Rai hiyo imetolewa Aprili 18,2025 na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Saidi Madito wakati wa semina iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mbeya iliyolenga kuwajengea uwezo na kubadilishana uzoefu katika utoaji huduma za kifedha na kushughulikia malalamiko na changamoto za huduma za kifedha.
Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mbeya Dkt.James Machemba amesema kuwa katika kuhakikisha usalama wa watumiaji na watoa huduma za kifedha, Benki kuu inatia nguvu katika maeneo matatu ambayo ni kuhakikisha Watanzania walio wengi wanafikiwa na kutumia huduma za kifedha, kuwalinda watumiaji wa huduma za kifedha na kuwajengea uwezo wa huduma za kifedha ili kuepuka malalamiko na uhalifu wa kifedha.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewapongeza Benki Kuu kwa kuona umuhimu wa kuandaa semina hiyo yenye lengo la kuwajengea uwezo Wadau ikiwemo vyombo vya usalama katika masuala ya huduma za kifedha.
Kamanda Kuzaga amesema kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kama mdau katika kushughulikia malalamiko na makosa mbalimbali ya kifedha litaendelea kushirikiana na wadau wengine ili kuzuia na kudhibiti uhalifu wa kifedha ikiwemo utapeli, wizi kwa njia ya mtandao na utengenezaji na usambazaji wa noti bandia katika mzunguko wa fedha.
Semina hiyo imeshirikisha wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, watumishi wa umma na wadau mbalimbali wanaoshughulikia changamoto na malalamiko dhidi ya watumiaji wa fedha Mkoa wa Mbeya.


More Stories
Polisi Mbeya kuimarisha ulinzi kuelekea sikukuu ya Pasaka
BAKWATA yawazawadia washindi wakuhifadhi Qur’an
Chalamila:Dar ni salama,aelezea mafanikio na mipango ya maendeleo ya Mkoa