Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema huwachukua na kuwalea katika mazingira yanayostahili watoto wanaotupwa au kutelekezwa,ili waweze kupata haki zao za msingi na siyo kuwa huwatenganisha watoto na familia zao.
Kauli imetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Anna Athanas Paul,katika kikao kilichofanyika Makao ya Watoto Kurasini jijini Dar es Salaam, baina ya Wizara hiyo, Wajumbe wa kamati ya Ustawi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Amesema Serikali imejenga nyumba ya kulea watoto ipo Mazizini lakini haiwatenganishi na familia zao, ila kwa wale watoto waliotupwa katika mabede ya taka hulelewa moja kwa moja na Serikali kwasababu hawana wazazi.
Ameeleza Zanzibar hakuna watoto wa mitaani isipokuwa kuna familia zenye mazingira magumu, ambazo huwatumikisha watoto katika biashara ndogo ndogo za kuuza mayai na vitu mbali mbali,lakini serikali huwa inakomesha vitendo vya kuwatumikisha watoto.
Hata hivyo ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto wenye umri mdogo kwani baadhi ya watu huwa ajiri kwa kazi za nyumbani kupika na kulea watoto wenzao.
Amesema sio kitendo kizuri kwani kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 anahitaji kupata haki zake za msingi ikiwemo elimu, malezi bora, matibabu, nk.
Amefahamisha kwamba watu wanaotaka kuwasili mtoto/watoto hupatiwa kupitia Wizara hiyo, ili watoto hao wakikua waone wana wazazi wao kama wengine.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Abeida Rashid amesema Zanzibar imepata eneo kubwa la kujenga kituo kikubwa cha kuwalea watoto ili waweze kuweka mazingira mazuri pamoja na kuingiza stadi za maisha ikiwemo kuwafundisha kilimo na ufugaji wa kuku kama walivyoshuhudia katika Makao ya Watoto kurasini.
Amesema SMZ inawalea watoto 26 katika nyumba ya Mazizini na inawapa huduma zote ikiwemo elimu, afya na malazi pamoja na fedha za matumizi mbalimbali ambazo hutolewa kila mwezi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Sabiha Filfil Thani, amehimiza masuala ya usalama na ulinzi kwa watoto kuwa yanatakiwa kuimarishwa wakati wote katika kituo.
Nae Meneja wa Makao ya Watoto Kurasini Twaha Kibalula, amesema makao hayo yalianzishwa mwaka 1966 na Serikali chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa lengo la kutoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi ikiwemo wenye ulemavu na waliopotezana na familia zao.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2023/2024 kituo kimehudumia watoto 209 kati yao wavulana 160 na wasichana 49, ambapo katika kati yao watoto 18 ni wenye ulemavu.
Ameeleza kwa sasa kituo kina watoto 82, na kinaendesha miradi midogo midogo ya uzalishaji mali kama ufungaji kuku na kilimo cha bustani ya mbogamboga ambazo husaidia katika mlo na kutatua changamoto za matumizi madogo madogo ya fedha yanapojitokeza.


More Stories
Vyombo vya ulinzi na usalama Mbeya,Benki kuu kushirikiana kutatua changamoto za utapeli mtandaoni
Polisi Mbeya kuimarisha ulinzi kuelekea sikukuu ya Pasaka
BAKWATA yawazawadia washindi wakuhifadhi Qur’an