April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Samia mgeni rasmi Tuzo za Waandishi wa habari za Maendeleo

Na Penina Malundo,Timesmajira

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Tuzo za waandishi wa habari za maendeleo zinazotarajiwa kufanyika Aprili 29,2025 katika ukumbi wa Mabele jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 15,2025,Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA),Dkt. Rose Reuben amesema tuzo hizo zinalenga kuhamasisha uandishi wa habari za maendeleo unaojikita katika kufanya uchambuzi na utafiti wa kina,kuongeza maudhui ya ndani,kuzingatia weledi,maadili na uwajibikaji wa kitaaluma,kukuza uzalendo na kujenga taswira chanya ya nchi.

Amesema tuzo hizo zinajulikana kwa jina la Samia Kalamu Awards zinatokana na mafunzo yaliyotolewa mwaka jana 2024 kwa lengo la kukuza na kuendeleza uandishi wa habari za maendeleo nchini.

”Walengwa wa tuzo hizi ni waandishi wa habari,wachapishaji wa maudhui ya mitandaoni ,maafisa habari,watangazaji na vyombo vya habari ambao walishiriki kwa kutuma kazi zilizorushwa ama kuchapishwa kupitia vyombo vyao,”amesema.

Amesema Tuzo hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu ikiwemo kundi linahusisha Tuzo Maalum za Kitaifa ambazo ni pamoja na Tuzo ya Chombo cha Habari Mahiri kitaifa,Tuzo ya Wnahabari Wabobevu,Tuzo ya Afisa Habari Mahiri wa Serikali,Tuzo ya Mwandishi wa Habari Mahiri Kitaifa na Tuzo ya Uandishi wa Habari za matumizi ya nishati ya safi ya kupikia.

”Pia kundi la Pili kuna Tuzo kwa Vyombo vya Habari ambavyo ni Tuzo za Televisheni ,Vyombo vya Habari Mtandaoni,Redio ya Kitaifa,Magazeti na Redio za Kijamii,”amesema

Aidha amesema kundi la Tatu la Tuzo hizo ni Tuzo za Kisekta zitakazotolewa kwa waandishi wa habari waliobobea katika kuandika makala za maendeleo kweye sekta mbalimbali ikiwemo afya ,maji,nishati,mazingira,jinsia wanawake na makundi maalum,ujenzi,viwanda na biashara,maliasili na utalii,mifugo na uvuvi,uchumi wa buluu,kilimo,utamaduni,sanaa na michezo,Tehama na Ubunifu,mazingira,ardhi na makazi,madini,fedha na uchumi,vijana na uwekezaji.

Kwa upande wake Mhandisi Mkuu Mwandamizi Kitengo cha Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jani Kaaya amesema washindi watatunukiwa zawadi mbele ya mgeni rasmi kama ishara ya kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika ustawi wa taifa.