Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
TIMU ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) imeendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi waliopata masahibu, baada ya Aisha Chogogwe (31), mkazi wa Kijiji cha Kwefingo, Kata ya Migambo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kutishiwa maisha kuwa atakatwa mapanga akitakiwa kuondoka kwenye nyumba baada ya mume wake kufariki.
Chogowe amedai baada ya mume wake kufariki Machi 11, 2021, mdogo wake na marehemu alimrithi , lakini baada ya miezi mitatu mama mkwe pamoja na mume mrithi, walimshinikiza kuondoka kwenye nyumba ya marehemu ili kijana huyo aweze kuoa mwanamke mwingine, lakini Chogogwe alikataa, kwa madai nyumba hiyo alijenga na mume wake na ana watoto nae wawili wa kike na kiume.

Chogogwe ameeleza hayo leo Aprili 14, 2025 mbele ya timu ya MSLAC ambayo ilikuwa inasikiliza changamoto mbalimbali za wananchi mjini Lushoto ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia na namna ya wananchi kupendelea kuandika wosia.
“Nimewatafuta watoa huduma za msaada wa kisheria ili mnisaidia kuishi kwa amani mimi na watoto wangu, kwani tangu nimefanyiwa fujo na mume mrithi ambapo tangu nimerithishwa kwake mwaka 2021, hatukuwahi kuwa na mahusiano mazuri. Na hata ugomvi aliounzisha nyumbani kwangu baada ya kuwa huko alikokuwa zaidi ya miaka mitatu, alikuja na kusema sipokei simu zake wakati yeye hana namba yangu wala mimi sina namba yake.
“Siku ya Aprili 6, mwaka huu alipokuja kunifanyia fujo nyumbani kwangu alisema wewe unajifanya mtawala hapa na hii nyumba nitaichoma moto, na nitakuua kama usipoondoka hapa. Huu mji ni wa kwangu na kakaangu sababu yeye ndiyo amejenga hivyo sitaki kumilikiwa na mtu, huku akipiga panga chini. Ndipo akapigiza redio chini, akavunja tv. Baadae baba yake alipokuja aliondoka nae, lakini wakati huo nilikuwa nimejificha kwa jirani. Mimi niliporudi nikafungasha watoto wangu Lucas (13) anaesoma darasa la saba na Agness (5) wa darasa la kwanza, tukahamia kijiji kingine kwa ndugu zangu”amesema Chogogwe.

Chogogwe amesema matatizo yalianza baada ya mume wake kufariki mwaka 2021, ambapo awali walimueleza ili kuishi kwenye nyumba aliyoacha mtoto wao ni lazima arithiwe, yeye akakubali, lakini baadae ilionekana hawataki kumuona kwenye nyumba ya mtoto wao.
“Shida ilianza kwa mama mzazi wa marehemu mume wangu kunitaka niondoke ili mtoto wake ambaye alinirithi mimi aoe mke mwingine. Nilimueleza mama mkwe, mimi siwezi kuondoka hapa sababu hapa ni kwangu, na siwezi kwenda kuwalea watoto ugenini wakati watoto wana nyumbani kwao. Na nyumba tulijenga mimi na mume wangu na hata vifaa vya ndani tulinunua wote, na mwaka huo 2021 alikuja nyumbani kwangu mara tatu kusema maneno hayo.
“Baada ya kumkatalia mama mkwe mimi kutoka kwenye nyumba yangu, mtoto wake ambaye alinirithi akatoka huko alikokuwa zaidi ya miezi mitatu akaja kunfanyia fujo kwa kunipiga na kuniumiza ubavuni. Nikaenda polisi nikachukua PF 3 nikaenda kutibiwa. Baada ya kutibiwa baba yake na mama yake waliitwa polisi, lakini mhalifu hakwenda wala mama yake, lakini baba yake alifika polisi” alidai Chogogwe.

Chogogwe alidai baada ya kuwashitaki wakwe zake aliporudi nyumbani alikuta kufuli lake limewekewa kufuli jingine ili asiweze kuingia ndani wakidai kwa nini amekwenda kuwashitaki, akawapigia simu polisi kuwaelezea tukio hilo, wakamueleza akatafute sehemu salama ya kulala, halafu asubuhi aende akafungue mashitaka mengine.
Baada ya baba kufika polisi na kuulizwa alipo mtoto wake ambaye amefanya uhalifu wa kumpiga mtu, akasema hajui alikokwenda, hivyo baba mkwe akawekwa ndani Kituo Kikuu cha Polisi Lushoto, na aliwekwa ndani siku mbili, lakini baadae alikwenda akaachiwa na maiaha yakiwa yanaendelea, huku mtoto wao akiwa amekimbia mji hadi aliporudi Aprili, mwaka huu, na kufanya uhalifu, na sasa anatafutwa tena.

Chogogwe ambaye ni mwanamke anaeishi kwa kulima vibarua, kusaidia fundi kujenga nyumba na kulima mboga mboga, anasema anataka mhalifu aliyemtishia maisha akamatwe, alipe mali alizoharibu, na wazazi wa marehemu waweze kuelimishwa kuwa ile nyumba ni yake yeye na watoto wake, na aweze kurejea kwenye nyumba hiyo ambayo ameifunga, na kuanza kuishi kwa ndugu huku akipata shida na watoto wake.
Mjumbe wa MSLAC ambaye pia ni Afisa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi Wilaya ya Lushoto, Mwajuma Shaaban aliwataka wanawake wasikae kimya wanapokutana na masahibu kama hayo ya kupigwa ama kunyanyaswa, kwani Chogogwe amefanya jambo la maana kwa kujitokeza badala ya kukaa, na baadae kupewa kilema ama kuuawa.
Afande Mwajuma pamoja na timu ya MSLAC waliweza kumpa msaada wa kisheria, na baadae alimsaidia kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Lushoto ili aweze kupata haki zake ikiwemo kurudi kwenye nyumba yake, kumfungulia mashitaka mhalifu, na kuweza kuwaelimisha wazazi wa marehemu.

More Stories
Dar yang’ara tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu
Mbunge ahoji ukamilishwaji miundombinu Vituo vya afya
Mbunge ataka safari za ndege kuanzia Dodoma