April 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Kabudi:Tanzania ndiyo nchi pekee yenye anuai kubwa ya utamaduni na Lugha Afrika

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee yenye anuai kubwa ya Utamaduni na lugha Barani Afrika.

Amesema kwa upande wa Lugha Tanzania ndiyo yenye makundi yote ya lugha mengi kuliko nchi yoyote Afrika.

Prof.Kabudi amesema hayo jijini hapa leo Aprili 14,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

“Tunamakundi ya lugha ya kibantu ukichukua Afrika ya Magharibi wote nibwa bantu,tunaweza kuwa na makabila 600 lakini wote ni wabantu.Lakini sisi tunamakabila ambayo asili yao ni kibantu,wengine ni Waniloti na Waniloti ni makundi mawili kwenye Mbuga yani Wamasai na wale wa kwenye mito Wajaruo.

“Lakini pia sisi tunao Wakoisani wapo Kondoa,Ovada mpaka Manyoni,lakini sisi pia tunawatu wanaozungumza lugha za Kiafloatiki ni Wairaq na Wamburu.

Vilevile amesema Tanzania ndiyo nchi ambayo inamshikamano na umoja mkubwa kuliko nchi yoyote barani Afrika Kusini mwa Sahara kwasababu Tanzania sasa ni Taifa siyo mkusanyiko wa makabila na Rais  Dkt.Samia Suluhu Hassan aliendeleza hilo.

“Lakini pamoja na umoja huo tunaouona bado sisi ndiyo wenye anuai kubwa ya Utamaduni na lugha ambazo hazifanani lakini tumewekwa pamoja kama Taifa.

Akizungumzia mafanikio ya wizara hiyo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita ametaja ni pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), Kufuzu kwa Timu za Taifa kwenye mashindano ya Kimataifa pamoja na Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Michezo kwa ajili ya Mashindano ya AFCON 2027 kwa gharama ya shilingi bilioni 161.977.

Kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo (BMT), Kuandaa Matamasha matatu ya Kitaifa ya Utamaduni, Mafanikio ya Siku ya Maadhimisho ya Kiswahili, Kufungua Fursa za Lugha ya Kiswahili duniani kote na kufungua Vituo vya Kufundisha Kiswahili Nje ya Nchi.

Pia Utoaji wa Mikopo kwa wadau wa Sanaa na Utamaduni, Ugawaji wa Mirabaha kwa Wasanii, Uhuishaji na Uendelezaji wa Tamasha la Serengeti Music Festival, Uanzishwaji wa Tuzo za Kitaifa za Ucheshi na Uendelezaji wa Tamasha la Tuzo za Filamu nchini.

“Wizara imefanikiwa Kuimarisha Ukusanyaji Mapato ya kazi za Sanaa, Kuanzisha Mradi mkubwa wa Ujenzi wa Sports and Arts Arena, Mradi wa Jumba Changamani la Filamu (Film Studio) na kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari nchini,”amesema Prof.Kabudi.