April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lushoto watakiwa kumuunga mkono Rais Samia kuimarisha elimu

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

WANANCHI wa Kata ya Mbwei,Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wametakiwa kuungana na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuona wanafunzi wanaoanza darasa la awali wanamaliza kidato cha sita.

Ni baada ya kuonekana kuwa baadhi ya wazazi wanafanya biashara ya watoto wao hasa wa kike kwenda Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya kufanya kazi za ndani, jambo linalofanya kata hiyo, wilaya na Taifa kukosa wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kuendeleza uchumi na ustawi wa Taifa lao.

Hayo yamesemwa leo Aprili 10, 2025 na
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Gloria Mdemu wakati anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Mbwei, Kata ya Mbwei akiwa na timu ya Kampeni ya Msaada ya Kisheria ya Mama Samia.

“Mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kila mtoto wa Kitanzania ana fursa sawa na mtoto mwingine yeyote wa Kitanzania katika masula ya elimu. Tumeanzisha Program ya Shule Salama kwa maana mtoto anapoanza darasa la awali anatakiwa afike kidato cha sita, na kama sio kidato cha sita, basi vyuo vya kati akiwa salama.

“Mbwei kumekuwa na changamoto kubwa sana upande wa watoto kwa baadhi ya wazazi kuwapeleka baadhi ya watoto hasa wa kike kwenda kuwa wafanyakazi wa ndani Mombasa nchini Kenya na miji mikubwa mingine ya Tanzania. Kwa hiyo kupitia kampeni hii ya Mama Samia, ninawaomba ninyi muwe mabalozi kwenda kuwaeleza wenzenu kuacha jambo hili” alisema Mdemu.

Mdemu alisema ulinzi na usalama wa mtoto ni jukumu la jamii kuanzia mzazi, mlezi, jirani,viongozi wa vijiji,kata,dini na Serikali na moja ya kuwalinda watoto wa kike ni kuhakikisha hawapati ujauzito, ama kufanyiwa vitendo vya ukatili, ambapo jambo hilo la ukatili hata watoto wa kiume wanafanyiwa.

“Mimba za utotoni imekuwa ni tatizo kubwa kwenye jamii yetu.Pamoja na kwamba kuna sheria inasema mtoto wa miaka 14 wazazi wakiridhia mtoto anaweza kuolewa, sisi tumekataa, na tunasema mtoto ni mtu yeyoye aliye chini ya miaka 18. Kwa hiyo mimba ya miaka 15, tutaanza na wewe mzazi maana tunahitaji hawa watoto wafike mbali, na ndoa za utotoni tunazikataa.

“Sio vizuri kila wakati mnaletewa viongozi kutoka mbali wakati utaratibu wa elimu ni huo huo Tanzania nzima. Kama tutawasomesha wa kwetu siku moja watarudi hapa hapa na kuwa walimu. Na hata kama hatarudi hapa bado atakuwa daktari, mhandisi ama Waziri au Mbunge. Si mnamuona mheshimiwa Profesa Riziki Shemdoe (Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi) anapokwenda Ngwelo, kule wana vituo vya afya na huduma nyingine. Amepata Ukatibu Mkuu sababu ya shule” alisema Mdemu.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Mbwei, Huruma Mwankuga, ambapo zaidi ya miaka mitano iliyopita shule hiyo iliwahi kuwa sehemu ya shule zilizofanya vibaya nchini, alisema kwa sasa wanajaribu kuimarisha ufundishaji na ufaulu ili watoto wanapomaliza darasa la saba, waweze kuendelea na sekondari na vyuo ikiwemo VETA.

“Mwaka 2020 ni wanafunzi wanne (4) ndiyo walikwenda sekondari, wavulana watatu na msichana mmoja kati ya wanafunzi 91. Mwaka 2021 waliokwenda sekondari ni wanafunzi 16, wavulana wanane na wasichana wanane, kati ya wanafunzi 115. Mwaka 2022, waliokwenda sekondari ni 13, wavulana tisa na wasichana wanne (4) kati ya wanafunzi 160. Mwaka 2023 waliofaulu ni 24, wavulana 11 na wasichana 13 kati ya wanafunzi 93, na mwaka 2024 waliofaulu ni 34, wavulana 12 na wasichana 22 kati ya 93..

“Tupo kwenye jitihada kubwa kwa kuhakikisha watoto wanasoma asubuhi na jioni, na walimu wanagawana wanafunzi wa darasa la saba ili kuwafundisha, na mwaka huu ambao wanafunzi wapo 60 tunataka kuona ufaulu unaongezeka” alisema Mwankuga.