Na Mwandishi Weu, TimesMajira Online, Zanzibar
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kuhakikisha watuhumiwa wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa watoto wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati alipomtembelea hospitalini mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13, anayelezwa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kijana anayefahamika kwa jina la Ramadhani Hamza Hussein (28), mkazi wa Tomondo, Unguja.
Tukio hilo linadaiwa kutokea katika eneo la Jang’ombe, Mjini Unguja, mnamo tarehe 1 Machi 2025, na baadaye kuripotiwa rasmi polisi tarehe 31 Machi 2025 katika kituo cha Mkono kwa Mkono.
Kwa sasa mtoto huyo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Lumumba, Zanzibar, huku taratibu za kisheria zikiendelea ili haki iweze kupatikana.

Serikali Yaonya Jamii
Akizungumza baada ya kumjulia hali mtoto huyo, Waziri Riziki Pembe ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema wanapobaini matukio au viashiria vya vitendo vya udhalilishaji kwenye maeneo yao.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda watoto dhidi ya watu waovu. Tukiona dalili zozote zisizoeleweka au matendo ya ajabu kwa watoto, tusisite kutoa taarifa kwa Sheha au Polisi ili hatua zichukuliwe haraka,” alisema Waziri Riziki.
Aidha, Waziri huyo amesema licha ya adhabu yoyote atakayopata mtuhumiwa, ukweli ni kwamba madhara aliyoyapata mtoto huyo kimwili na kisaikolojia ni makubwa na hayawezi kufutika kwa urahisi.
“Mtuhumiwa anaweza kufungwa hata miaka 100, lakini bado hatuwezi kurudisha thamani na utu wa mtoto wetu,” alisema kwa masikitiko.

More Stories
Polisi kuchunguza madai ya mwanafunzi kutupa kichanga chooni
Sekiboko ahimiza uwekezaji Elimu ya ufundi
Wazee wawili jela maisha kwa kubaka na kulawiti