Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online,Shinyanga
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) umetajwa kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri kwa asilimia nane huku ukiongeza uwezo wa kaya kumudu gharama za mahitaji ya msingi kwa asilimia 10.
Hali hiyo imeelezwa katika mkutano mkuu wa kawaida wa wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Shinyanga (SPC) na Christopher Kidanka ambaye ni Ofisa Habari na Mawasiliano kutoka Makao Makuu ya TASAF.

Kidanka amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) bila ya uwepo wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini hapa nchini kiwango cha umaskini cha jumla kingekuwa ni asilimia 8, 9.2 au juu zaidi ya kilivyo hivi sasa, huku umaskini wa kipato ukiwa asilimia 7 juu zaidi.
Amesema ili kupima matokeo ya utekelezaji wa TASAF ilifanyika tathimini ambayo ilionesha,mpango umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya walengwa na kupunguza kiwango cha umaskini.
“Baadhi ya matokeo ni kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri kwa asilimia 8,kwa kuongeza uwezo wa kaya kumudu gharama za mahitaji ya msingi ya kaya kwa asilimia 10,kuongezeka kwa idadi ya walengwa wanaoshiriki katika shughuli za kilimo na ongezeko la matumizi ya pembejeo ambazo zinaongeza tija kwenye uzalishaji,”amesema nakuongeza:
“Pia ongezeko la uandikishwaji na mahudhurio shuleni kwa watoto kutoka kaya maskini kwa asilimia 6,”.
Kuhusu kuwaandaa walengwa ambao wamekaribia kuondoka kwenye mpango huo baada ya uchumi wao kuimarika, amesema hadi kufikia Machi 2024, Tanzania Bara walengwa 27,964 kutoka Halmashauri 33 walipatiwa mafunzo na ruzuku ya uzalishaji ya kiasi cha shilingi bilioni 8.6.
Ambapo kiasi cha shilingi bilioni 8.9 kilitolewa kwa walengwa 23,399 upande wa Unguja na Pemba,fedha ambazo ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yao ya kuzalisha na kuongeza kipato cha kaya.
“TASAF tunaamini kwamba ili kukata mnyororo wa umaskini tunapaswa kuwa rasilimali watu yenye uwezo. Kwa hiyo kutokana na makubaliano tuliyoingia na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), wahitimu wenye sifa ya kujiunga na elimu ya juu kutoka kaya ambazo zipo kwenye mpango hupatiwa mikopo asilimia 100,”amesema na kuongeza:
“Na kwa wengine ambao hawafikii ngazi hiyo huunganishwa na afua nyingine za Serikali za kukuza ujuzi,ili waweze kuajirika na kujiajiri ambapo kufikia sasa jumla ya wanafunzi 11,524 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamenufaika na mikopo hii,”.

Pia ameeleza mafanikio ambayo yamepatikana katika nyanja nyingine ikiwemo ongezeko la matumizi ya huduma za afya miongoni mwa kaya za walengwa na kuongezeka kwa mahudhurio kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa watoto wenye umri kati ya miezi 0 hadi 24 kutoka kaya maskini.
Kuongezeka kwa akiba na rasilimali za kaya ambazo zinawezesha kujikinga na majanga yanapotokea, kuboresha makazi kwa kujenga nyumba bora kwa kutumia matofali ya kuchoma au saruji na kupaua kwa mbao na kuziezeka kwa bati.
“Hivi sasa TASAF inafikia kaya 1.3 milioni katika Halmashauri zote nchini,ambapo kila kaya ina wastani wa wanakaya wanne hivyo wananchi wanaofikiwa moja kwa moja na TASAF ni zaidi ya milioni tano, mfano kati ya Januari na Juni 2024 pekee zaidi ya shilingi bilioni 945 ziliwasilishwa kwa walengo wa mpango,” ameeleza.

More Stories
Boshe:ALF imekutana kutambua Maendeleo Endelevu ya Bara la afrika
Kikwete:Afrika yazidi kusonga mbele,mafanikio kuanza kuonekana
Diwani awapa bima za afya watoto wa mahitaji maalum