Na Penina Malundo ,Timesmajira
Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete anatarajia kuungana na marais wengine watatu na baadhi ya viongozi Wakuu barani Afrika kwenye Kongamano la nane la Kikanda la Viongozi Afrika linalotarajiwa kufanyika Aprili 7 na 8 mwaka huu Kampala, Uganda.
Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mahusiano kwa Umma, Taasisi ya Uongozi Suzana Aroko alisema kongamano hilo limeandaliwa na taasisi ya Uongozi ambalo litajadili mada nne ikiwemo Kutokomeza umaskini na kukuza uchumi, Afya bora na ustawi, Kuimarisha elimu na ujuzi pamoja na kujadili Mifumo madhubuti na endelevu ya kusimamia mazingira barani Afrika.
Amesema miongoni mwa marais hao ni pamoja na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Tunisia Dkt. Mohamed Moncef Marzouki, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Sierra Leone Dkt. Ernest Bai Koroma pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye ndiye atakuwa mgeni rasmi na anatarajia kufungua kongamano hilo.

Aidha amesema kongamano hilo linalenga kutoa fursa ya kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji,changamoto, na namna ya kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu barani Afrika.
Amesema malengo mahususi ni Kujadili hatua zilizofikiwa na nchi za Afrika katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, kuainisha changamoto zinazokwamisha utekelezaji, kutengeneza mipango inayotekelezeka kwa ajili ya kutatua changamoto katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
“Kongamano hili linaitishwa na Rais Mstaafu Kikwete ambaye pia ni Mlezi wa Kongamano pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Hailemariam Dessalegn Boshe.

“Malengo mengine mahususi ni kuhamasisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya nchi za Afrika pamoja na kuleta mbinu zenye ubunifu na kuimarisha mashirikiano kwa ajili ya kuchochea maendeleo endelevu,”Amesema Aroko
Hata hivyo amesema washiriki wengine ni viongozi waandamizi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na sekta zote ikiwemo sekta ya umma, l binafsi, sekta ya elimu ya juu, na sekta ya asasi za kiraia.
Kuhusu Taasisi ya UONGOZI, Aroko alisema ni taasisi ya kikanda ya kuimarisha kada ya uongozi iliyo chini ya Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ilianzishwa mwaka 2010 na Serikali za Tanzania na Finland kwa lengo la ya kujenga na kuimarisha viongozi wa Afrika ili kukidhi matakwa ya ndani ya kutoa huduma kwa wananchina kuyafikia maendeleo endelevu.
Amesema kongamano hilo ni tukio muhimu litakalofanyika kabla ya Mkutano wa 11 wa Kikanda wa Maendeleo Endelevu wa Aprili 9 hadi 11, 2025, unaoratibiwa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi Barani Afrika(UNECA).
More Stories
Diwani awapa bima za afya watoto wa mahitaji maalum
Rais Mwinyi:Tuzindue mpango wa ujuzi kwa vijana katika uchumi wa buluu
Dkt.Mpango ashiriki dua,kumbukizi miaka 53 ya Hayati Karume