April 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msigwa :Wakuu wa mikoa andaeni maeneo ya upandaji miti

Na. Mwandishi Wetu ,Timesmajira, Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewaomba wakuu wa Mikoa ambao maeneo yao itafanyika mikutano ya maafisa habari kuandaa maeneo kwa ajili ya shughuli ya upandaji miti ili kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya uhifadhi wa mazingira.

Msigwa amesema hayo leo Aprili 05, 2025, wakati akiongoza maafisa habari wa Serikali katika zoezi la upandaji wa miti 2000 katika msitu wa Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar lililoshuhudiwa pia na Mkuu wa Mkoa huo Ayoub Mohammed Mahamoud.

Amesema maafisa hao watakuwa sehemu ya zoezi hilo muhimu la utunzaji na uhifadhi wa mazingira ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais,Dkt. Samia Suluhu Hasssan za kutunza na kuhifadhi mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Sisi kama maafisa habari wa Serikali nchini ni lazima tuwe sehemu ya kutengeza nchi ya kijani na hilo litawezekana kwa kushiriki katika zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini” amesisitiza Msigwa.

Ameeleza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu ili kuunga mkono kwa vitendo jitihada za kutunza na kuhifadhi mazingira na kuifanya Tanzania kuwa ya kijani.

Maafisa Habari hao wa Serikali wapo visiwani Zanzibar kushiriki Kikao Kazi cha 20 cha siku 4 kilichoanza Aprili 03, 2025 ambacho kinatarajiwa kuhitimishwa Aprili 06, 2025.