April 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Nchimbi: Uchaguzi upo palepale hakuna mwenye mamlaka ya kuzuia

CHADEMA isiposhiriki uchaguzi huu itashiriki chaguzi zingine

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi,huku akisisitiza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utafanyika kama kawaida kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika Aprili 4, 2025 mkoani Ruvuma, Balozi Nchimbi amesema, tangu nchi ipate uhuru hakuna mtu, chama wala mamlaka zozote za kiserikali zenye uwezo wa kuzuia uchaguzi usifanyike.

“Nchi yetu imekuwa na utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano,na ninyi nyote mnafahanu hilo, hakuna mtu yoyote si Rais wa nchi, Makamu wa Rais wala Waziri Mkuu anayeweza kuzuaia kufanyika kwa uchaguzi.Hata kama kitashiriki chama kimoja kwenye uchaguzi basi zitapigwa kura za ndiyo na hapana na utaratibu huo umezingatiwa tangu enzi,”amesema Balozi Nchimbi.

Aidha Balozi Nchimbi akizungumzia kampeni zinazofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya ‘No Reform,No Election’, amesema, huo ni uamuzi wa chama husika kuamua kutoshiriki katika uchaguzi mkuu,hivyo amewataka Watanzania waheshimu maamuzi ya chama hicho ya kutotaka kushiriki kwenye uchaguzi mkuu huku akiendelea kumsisitiza kuwa Uchaguzi bado utafanyika na vyama vilivyotayari vitashiriki.

“Naomba niwahakikishie Watanzania wote kuwa uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani utafanyika kama kawaida.Vyama vinavyodai kuwa havitashiriki uchaguzi tusivilazimishe, CHADEMA kama wanasema hawatashiriki kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 ni sawa, ni haki yao, bado wana muda watashiriki kwenye chaguzi zingine mwaka 2030, 2035, 2040, 2050 na kuendelea,”ameeleza Balozi Nchimbi.

Sanjari na hayo, Balozi Nchimbi,ameviomba vyombo vya habari kuzingatia weledi katika kuchakata taarifa na kutoa katika vyombo vyao kwa ajili ya maslahi ya wananchi,kwani zipo baadhi ya habari hazifai kutolewa zinaweza sababisha machafuko kwa Taifa.

“Niwaombe ndugu zangu Wahariri, tuwe tunachuja aina za taarifa ambazo tunataka kuzirusha katika vyombo vyetu kwani taarifa zingine hazifai na zinaweza kuleta mchafuko katika nchi yetu, hivyo tukiona taarifa kama hizo tuzipuuze na kuona ni kama chizi mmoja tu amepiga”, amesema Nchimbi.