April 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Umuhimu wa kujadili mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya watoto

Judith Ferdinand

Kwa mujibu wa Shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza(MYCN),linasema jamii bado  haijatambua umuhimu wa kujadili mabadiliko ya tabianchi kwa kushirikisha watoto,kwani inaamini kuwa athari za mabadiliko hayo zinawaathiri watu wazima pekee na siyo watoto.

 Ripoti ya mabadiliko ya tabianchi  kwenye haki za binadamu iliotolewa na Kituo cha Sheria  na Haki za Binadamu(LHRC), na kuzinduliwa Mei,2023,imebainisha kuwa afya,chakula,elimu ,maji safi na salama,mazingira,faragha na familia zimetajwa   kama haki zinazoathiriwa zaidi na  mabadiliko ya tabianchi huku kundi la watoto na wanawake likitajwa kuathirika zaidi.

Maandiko matakatifu yanasema”Mlee mtoto katika njia impasayo,naye hataicha hata atakapokuwa mzee”huku waswahili wakisema “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”,maneno haya  yanaungwa mkono na MYCN shirika ambalo linaamini kuwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sasa na miaka ijayo watoto wanastahili kupatiwa elimu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo wakiwa bado wadogo.

 Timesmajira Online,inafanya mahojihano na MYCN,ambao wanazungumzia umuhimu wa kujadili na kuwashirikisha watoto katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuifanya Tanzania kuwa ya kijani.

Mwanahabari mtoto kutoka MYCN,Bryton George, anasema,mtoto akipewa elimu ya mabadiliko ya tabianchi tangu akiwa mdogo  itatusaidia taifa na dunia kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko hayo na kufanya dunia kuwa sehemu salama.

“Mtoto akipewa elimu akiwa mdogo, elimu hiyo  haitoishia kwake lazima ataenda kuwambia na watoto wengine na hata watu wazima kutokana na tabia za watoto huwa hawakai na jambo pekee yao.Hivyo elimu hiyo  itasambaa  kwa haraka  na  jamii watajua  sababu na namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,”anasema Bryton.

Pia anasema, watoto ni taifa la kesho,hivyo mtoto akipewa elimu angali mdogo  itamjengea  utamaduni wa kupanda miti na kutunza mazingira ata atakapokuwa mkubwa.

“Mtoto akiwa na uelewa tangu mdogo kuwa akikata miti ovyo kunasababisha mvua kutokunyesha hivyo kuchangia ukame na ili aweze kukabiliana na mabadiliko hayo anapaswa kutunza mazingira na kukata miti kwa kufuata utaratibu mfano kata mti panda mti,atakikua tabia hiyo itakuwa ni muendelezo na itakuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku,”.

Hata hivyo Bryton,anasisitiza kuwa, ni rahisi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi endapo jamii,Serikali na wadau mbalimbali wataona umuhimu wa watoto kuwa sehemu ya kukabiliana nayo kwa kuwajengea uelewa pamoja na kutumia kumbukizi ya siku za kuzaliwa kupanda miti na kuitunza.

Kwa upande wake  Ofisa Mradi wa  ustahimilivu endelevu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto Mwanza kutoka MYCN Nuru Masanja,anasema,shirika hilo  linaona umuhimu wa kujadili mabadiliko ya tabianchi kwa watoto, kwa sababu wanajua wanapopandikiza elimu kwa watoto wakiwa  bado wadogo  kwanza itasaidia kubadili  mitazamo hasi kwa jamii kwani kadri wanavyokuwa ndivyo wanavyozidi kuwa na uelewa zaidi na binu za kukabiliana na mabadiliko hayo.

Kwani  watu wazima wamekuwa na mitazamo hasi kuhusu mabadiliko ya tabianchi nchi mfano jua lisipo chomoza wanahisi  ni mambo ya mila na desturi.

“Watoto  ni wepesi  kuchukua hatua tangu akiwa mdogo mpaka katika utu uzima,hivyo itasaidia kupunguza mitazamo ya watu kuhusu kuwa mabadiliko ya tabianchi yanasababishwa na mila na desturi,unavyompa mtoto elimu akiwa mdogo anaisamba kwa wenzake  na jamii.Wana uwezo wa kubadilisha fikra za familia na jamii nzima juu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,”anasema Nuru.

Pia  anasema,mtoto anapopewa elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi,“Tunamjenga katika utekelezaji  akiwa mdogo ni rahisi kufanya utekelezaji na kuchukua hatua ya jambo husika,mwisho wa siku inakuwa mazoea na kadri siku zinanvyozidi kwenda anaona ni kawaida na utamaduni wake kufanya vile anavyopaswa kufanya, kuliko kumbadilisha mtu mzima  mtazamo  wa kufanya kitu fulani wakati  amezoea kufanya jambo fulani  tangu akiwa mdogo inakuwa ngumu,”.

Ambapo anasisitiza kuwa kama mtoto amezoeshwa kupanda miti jambo hilo atakuwa amezoea na kuona ni sehemu ya maisha yake kufanya hivyo lakini  mtu mzima ukimpa elimu ya upandaji miti atapanda ila haita kuwa mazoea kwa sababu amekua katika mitazamo tofauti na hiyo hivyo hata kuitunza itakuwa ni kama adhabu.

Aidha anasema,mtoto akifundishwa kufanya usafi akiwa mdogo au jambo lolote linalohusu masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kutenga taka taka,anakuwa ameisha zoea  hivyo  atakua na tabia  ya kufanya hivyo ata akikua bila kuhitaji msukumo au hamasa kutoka sehemu nyingine.

“Hivyo kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamjengea mtoto mfumo wa kujitegemea katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi,lakini mtoto ana nguvu na uungwaji mkono  mfano ukimpa elimu ya mabadiliko ya tabianchi anao uwezo wa kumshawishi na kumbadilisha mtu mzima,kuliko mtu mzima kuelimishwa na mtu mzima mwenzie,”.

Nuru anasisitiza kuwa,elimu ya mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kwa watoto,kwani wao ndio wanaathirika sana bila wao kujua huk akitolea mfano,kunapofanyika shughuli za kibinadamu kunaweza kusababisha ongezeko la joto hivyo mvua kukosekana na kuwa na jua kali kupita kiasi,athari zake azimuathiri mtu mzima pekee pia na watoto.

Anasema mtoto,anaposhindwa kwenda shule kwa sababu ya mvua nyingi anaona ni kawaida ila anakua amepunguza siku za kuhudhuria masomo zilizowekwa na Serikali katika kalenda ya masomo kwa mwaka ambazo ni siku 194.

Hatua ambazo MYCN inafanya kushirikisha watoto

Nuru anasema,shirika hili limekuwa likichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia watoto elimu juu ya mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kukabiliana nayo kwa vitendo angali wadogo.

Ambapo kupitia mradi wa Ustahimilivu endelevu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto Mwanza unaotekelezwa na  MYCN  kwa ufadhili wa shirika la Sustainable Energy kutoka nchini Denmark,unaofanyika kwa Wilaya za Ilemela  kata sita  na Nyamagana Kata 11huku wahusika wakuu wa utekelezaji wake ni ni watoto hususani  wanahabari watoto na baraza la watoto.

Kupitia mradi huo wamefanikiwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya midahalo kwa baadhi ya shule juu ya mabadiliko ya tabianchi,elimu ya umuhimu wa kupanda miti kwa wanafunzi  na mpaka sasa wameweza kutoa miti 500 kwa shule tano ambayo wanafunzi wa shule hizo walishiriki kupanda na sasa wanaitunza.

“Tunaichochea  elimu ya mabadiliko ya tabianchi  kwa watoto sababu tunajua ni watu muhimu katika kubadilisha na wanachochea  mabadiliko kuliko watu wazima.Mtoto akitaka kubadili kitu anabadilisha kwa kiwango kikubwa kuliko mtu mzima ndio maana tunasema  mtoto ana haki ya kupata elimu hiyo akiwa mdogo na apandikiziwe kama mbegu,kwani kadri anavyozidi kukua hali ile inaendelea na kufanya kuwa utamaduni wake na hatoweza kusahau,”.

Hata hivyo ,shule ya msingi Magaka,iliopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,wameweza kuonesha umuhimu wa watoto kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuhakikisha wanapanda miti ambayo baadhi ilitolewa na MYCN.

Mmoja wa wananfunzi wa   shule ya msingi Magaka,Katibu Msaidizi wa Klabu ya Mzaingira  ya shule hiyo,Angel Chacha,amesema wanafunzi shuleni hapo  wanashirikishwa katika suala zima la upandaji wa miti na kuitunza, kufanya usafi wa mazingira na kufukia baadhi ya maeneo ya shule ambayo udongo wake umemomonyoka kutokana na mvua nyingi.

Katibu wa Klabu ya Mazingira shule ya msingi MagakaFides Samweli,amesema wanashirikishwa kupanda miti na kutunza mazingira shuleni hapo,ili kutengeneza kizazi chenye uelewa wa kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabaianchi.Na hapo mbeleni kufanya suala la utunzaji mazingira kama utaratibu wa kawaida na siyo shuruti.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Magaka,Mshongo Mmbaga,anasema, shule inawafundisha na kuwashirikisha katika wanafunzi katika  suala zima la upandaji miti shuleni na nyumbani,ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa sasa ni janga la dunia.

Wanafunzi ni wadau wazuri katika suala zima la upandaji miti,na hapa shuleni walikuja wadau kutupatia miti,tuliwakabidhi kila mtoto ana  mti wake ambao aliupanda na kuitunza,na  kwa sasa shuleni hapa  ipo  zaidi ya miti 100 ya matunda na kivuli.

“Watoto ni watekelezaji wa zuri wa mambo,tuwape kazi watoto ya kupanda miti ata miwili au mitatu ndani ya familia pamoja na kuwafundisha namna ya kuitunza,itasaidia kuondokana na changamoto hiyo,kwa jiografia ya Mwanza maeneo yake kuwa na milima na mawe,ipandwe miti ya asili ambayo inaweza kuota vizuri katika maeneo hayo,mfano hata hapa shuleni kuna eneo lina mawe lakini kuna miti ambayo ukiisha ipanda mizizi yake ikapenya haina shida inakuwa vizuri,”anasema Mwalimu Mmbaga.

Ofisa Elimu Watu Wazima Divisheni ya awali na msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Magembe Masalu,amesema,kuwafanya watoto kuwa sehemu ya mabadiliko ya tabianchi kunaweza kusaidia kufanikisha jambo hilo.Kwanza kuwafundisha wakatambua  namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo, kwa kujua kitu gani kinatakiwa kifanyike na wao wakashiriki  hasa kufanya mambo ya usafi wa mazingira,upandaji wa miti na maua hasa kwenye maeneo  ya shule na nyumbani.

“Halmashauri ya  Manispaa ya Ilemela, tumeanza  mchakato wa uboreshaji na utunzaji wa mazingira kwa kushirikisha wananfunzi/watoto, kupanda miti.Kila mwaka tunajitahidi kupanda miti zaidi ya miche 10,000 kwenye maeneo yetu ya taasisi za elimu msingi na sekondari,’amesema Magembe.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Mashelo Makila,amesema wanawasisistiza watoto na vijana  kupanda miti kuanzia shuleni na  kwenye familia zao.

Amesema watengeneza sera  na watunga sheria,watengeneze sheria  ambazo zitamfanya mwanafunzi anapotoka shuleni na kwenda nyumbani,akutane na kitu kile kile ambacho kinamfanya awe sehemu ya mapambano ya mabadiliko ya tabianchi.

 “Sheria iwepo ambayo ina lazima kila familia  inakuwa na miti angalau mitatu ambayo wameipanda ili kuhakikisha mabadiliko ya tabianchi  yanaondoka,kwa kufanya hivyo itatoka kwenye sheria na kuwa sehemu ya maisha  kama tabia,tamaduni ya watu kujijengea kuwa na miti katika maeneo yao na kuitunza tangu wakiwa wadogo,”.

Ofisa Mazingira Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, David  Mgunda,amesema njia kuu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kurejesha uoto wa asili  katika uso wa dunia na kuifanya kuwa ya kijani.Hivyo kitu wanachokifanya kwa sasa ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu namna ya kukabiliana na  mabadiliko ya tabianchi  pamoja na kuwashirikisha katika suala zima la upandaji miti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Amesema,mwaka 2022/2023,miti 39,700,waliipanda katika  taasisi mbalimbali ikiwemo shule za msingi na sekondari,vituo vya afya,zahanati na hospitali na kwa kiasi kidogo maeneo ya wananchi binafsi.Huku mwaka 2023/2024,miti takribani 40,727,ilipandwa katika taasisi hizo,asilimia 80  ya miti hiyo ilipandwa  kwenye shule.

“Walimu  waendelee kusimamia klabu za mazingira shuleni huku wanafunzi waendelea kuitunza na kupanda  miti katika maeneo ya shule na nyumbani,huku mazingira liwe somo la kujitegemea na lifundishwe kwa vitendo zaidi,”.

 Picha

WAOO10, Ofisa Mradi wa  ustahimilivu endelevu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto Mwanza kutoka MYCN Nuru Masanja,akitoa elimu ya mabadiliko ya tabianchi kwa wanahabari watoto wa shirika hilo.