Na Mwandishi wetu,Timesmajira
▪️Ni utekelezaji wa maagizo ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan
▪️Kiwanda cha kuchakata madini ya shaba chajengwa Wilayani Chunya,
▪️Serikali yaahidi kuwezesha viwanda zaidi vya uongezaji thamani madini
▪️Wachimbaji wadogo kunufaika na soko la uhakika la Madini Shaba
Kufuatia utekelezaji wa Mkakati wa kutosafirisha madini ghafi nje ya Nchi, Serikali yapongeza Wadau kwa kuitikia wito wa Mhe. Rais Dkt. Samia S. Hassan wa kujenga viwanda vya uongezaji thamani madini nchini.
Hayo yemesemwa leo na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipotembelea kujionea ujenzi wa kiwanda cha uongezaji thamani madini ya shaba kilichopo Kata ya Mbugani Wilayani Chunya kinachomilikiwa na Kampuni ya Mineral Access System Tanzania (MAST).
“Mhe. Rais ametuelekezaee kuhakikishia tunasimamia Sheria na Kanuni ili kuwezesha madini kuongezwa thamani hapa nchini kabla yayajasafirishwa nje ili nchi kunufaika na sekta ya madini.
“Tutaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa wadau na wawekezaji wengine walio tayari kuunga mkono jitihada hizi za Mhe. Rais ili kama Nchi tupate manufaa zaidi ya kiuchumi ikiwemo kuongeza upatikanaji wa ajira kwa wananchi wetu na kukuza pato la Taifa” amesema Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa madini ya shaba yanahitaji kuongezwa kiwango kwa kuchakatwa kufikia asilimia 20 au zaidi ili yaweze kuuzwa nje, Ile hali madini yanayopatikana nchini yana kati ya asilimia 0.5 mpaka asilimia 2, na kwamba kiwanda kitakuwa kinazalisha shaba kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 70, ambapo alisisitiza ni mageuzi makubwa sana ya kiuchumi nchini.

Vilevile, Waziri Mavunde aoneshwa kufurahishwa na mpango wa Kiwanda cha MAST wa kuhudumia wachimbaji wadogo kupitia kutoa elimu, kugharamia uchimbaji na kuwa soko la shaba yao ya kiwango cha chini ambayo awali walikuwa wakihangaika na soko. Hili litakuwa ni suluhisho tosha kwa wachimbaji wadogo kwani nguvu zao hazitakwenda bure.
Akisisitiza mikakati ya Serikali kwa wachimbaji wadogo, Mavunde amebainisha kuwa Wizara ipo mbioni kuanzisha Vituo vya ukodishaji wa mitambo ya uchimbaji Nchi nzima ili kusogeza huduma hiyo kwa wachimbaji wadogo na kwa gharama nafuu.
Awali, akimkaribisha Waziri katika kiwanda hicho, Georgefrey Kente, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MAST ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuahidi kwamba Kampuni yake inakwenda kujenga viwanda vingine kama hivyo katika Mkoa wa Dodoma na Lindi ili kufikia malengo yao ya uzalishaji.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Chunya ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya, Michombero Anakleth ameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa kiwanda hicho kwa kasi kubwa na kueleza bayana kuwa Uongozi wa Wilaya ya Chunya unaunga mkono kwa asilimia 100 zoezi la ufutaji wa leseni za madini zisizoendelezwa ili wapewe wawekezaji wenye nia njema kwa manufaa ya Nchi yetu.
More Stories
Polisi Mbeya yajivunia miaka minne ya mafanikio
Wahariri wa vyombo vya habari nchini wapongezwa
NCHIMBI: Nia ya CCM ni kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini