Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Bumbuli
Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Yusuph Makamba (87) amesema yupo tayari kujitolea kuzunguka nchi nzima ili kuwashawishi wazee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpigia kura katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Amesema Rais Dkt. Samia hakuja hapa duniani kwa ajili ya maslahi yake na familia yake tu, bali kwa ajili ya Watanzania wote, na kazi zake zinaonekana kuanzia huduma za jamii, miradi ya maendeleo, uchumi wa kaya na mtu mmoja mmoja.

Ameyasema hayo Aprili Mosi, 2025 kwenye Maulid ya kumbukumbu ya miaka 40 tangu kifo cha Baba yake mzazi Rajabu Makamba,ilioambatana na dua ya kumuombea Rais Dkt. Samia, yaliofanyika Kitongoji cha Kwemchungwa, Kijiji cha Mahezangulu, Halmashauri ya Bumbuli.
“Tulisha sema 2025 ni Samia,leo Watanzania wana amani, wana furaha kwa ajili ya Mama Samia, mkono wake umewagusa wengi ikiwemo wakina mama kuwatua ndoo kichwani.Chanda chema kinavikwa pete, sisi tunampa zawadi gani ni kura,”amesema Makamba na kuongeza:
‘Mimi kama Mzee wa Mkoa huu wa Tanga,tutampa kura. Na pamoja na uzee wangu huu kama mahali kuna wazee wakorofi, nitume nitakwenda,hata kama wazee wakorofi wapo Tabora, nitakwenda,”.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdulrahman, amesema CCM wameshamaliza kazi kwa kumteua Dkt. Samia kupeperusha bendera ya chama hicho kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu 2025.
Ambapo amesema,hawakumteua kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na uwezo wake ambao ameonesha kwa miaka minne ya uongozi wake, na Mkoa wa Tanga ni mashahidi, kwani wao wamefaidika zaidi.
“Rais Dkt. Samia amekusudia kuufungua Mkoa wa Tanga kwa miradi mbalimbali ya kimaendeleo na ameelekeza tuufungue Mkoa wa Tanga kwa suala zima la viwanda pamoja na mikakati ifanyike na inaendelea hapa Lushoto na Jimbo la Bumbuli kuinua zao la chai ambapo kwa Lushoto ni sehemu ya uchumi wetu, ili kupata soko nje, na kujenga kiwanda kingine ukiacha kilichopo sasa Mponde,”amesema Abdulrahman.
Sheikh wa Kata ya Kerenge na Mkuu wa Chuo cha Kiislamu (Mudri) cha Alfalaha kilichopo Matalawanda, Kata ya Kwemazandu wilayani Korogwe, Alhaji Zakaria Baruti,amesema Rais Dkt. Samia ameonesha ukomavu, uvumilivu na upendo kwa wananchi wake, hivyo Watanzania hawana cha kumlipa bali kumuombea dua.

.

More Stories
Polisi Mbeya yajivunia miaka minne ya mafanikio
Wahariri wa vyombo vya habari nchini wapongezwa
NCHIMBI: Nia ya CCM ni kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini