March 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasira atoa siku 14 mnunuzi wa kahawa kulipa zaidi ya milioni 600 za wakulima

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven Wasira, ameiagiza kampuni ya GDM ambayo ni mnunuzi wa kahawa kuhakikisha inalipa madeni yote ya wakulima wa kahawa Wilaya ya Rungwe ndani ya siku 14.

Kauli hiyo ametoa baada ya malalamiko ya wakulima hao kuwasilishwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Machi 18, 2025, stendi ya mabasi ya Mji Mdogo wa Tukuyu.

Wakulima hao ambao wanadai malipo ya zaidi ya milioni 600 kutoka kwa kampuni hiyo, wamesema ucheleweshaji wa malipo umewaathiri kwa kiasi kikubwa, huku wengi wakikosa fedha za kugharamia mahitaji yao na kuendeleza uzalishaji wa chai.Pia kudhindwa kulipa ada za shule za watoto wao na kudhindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Akizungumza katika mkutano huo, Wasira amesisitiza kuwa Serikali haipo tayari kuvumilia ucheleweshwaji wa malipo ya wakulima, huku akitoa onyo kali kwa kampuni hiyo kuhakikisha inatekeleza agizo hilo ndani ya muda uliopangwa.

“Natoa siku 14 kwa mnunuzi wa chai wa GDM kuhakikisha wakulima wote wanalipwa haki yao bila visingizio, wakulima hawa wamefanya kazi yao na wanapaswa kuheshimiwa kwa kulipwa kwa wakati,” amesema Wasira.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, amesema lengo la chama hicho ni kutatua kero na changamoto za wananchi,kusimamia haki na usawa.

Pia amesema,Mkoa huo utahakikisha unaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha matumizi ya 4r yanatumika ipasavyo ili kuendelea kujenga nchi yenye amani.