Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Kibaha
MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa,amesema mchakato wa ujenzi wa barabara ya haraka ya Kilomita 78.9, Kibaha-Chalinze,majadiliano yanaendelea kati ya Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) na mbia, ili kupata mradi unaoendana na thamani ya fedha.
Ambapo barabara hiyo itatekelezwa kwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPP),ambayo itakuwa ya kulipia
Akizungumza Kibaha Mkoani Pwani baada ya kutembelea Kongani ya viwanda ya Sino-Tan iliyopo eneo la Kwala, Msigwa amesema, utekelezaji huo unafanyika baada ya Serikali kufanya marekebisho katika sheria ya PPP sura namba 103.
Hii ni pamoja na kanuni zake za mwaka 2020 na marekebisho ya mwaka 2023, ili kushirikisha sekta binafsi katika miradi ya kimkakati ya maendeleo.
“Tumefanya hivi kutokana na ukuaji wa mahitaji ya miundombinu ya barabara nchini, Serikali imeamua kutumia njia ya ubia kwa kushirikisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ili kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi hii,”amesema Msigwa.
Pia amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23, Serikali iliridhia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya haraka ya kulipia kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro Km 163.8.
“Baadhi walishaanza kusema mpango umefeli,mpango haujafeli, Serikali inafanya maandalizi ili utekelezaji wake usije kuleta changamoto nyingi baadaye na sasa utekelezaji wa mradi huu umegawanywa katika sehemu mbili,” amesema Msigwa.
Awamu nyingine ni barabara ya Chalinze-Morogoro,itakayokuwa na urefu wa Kilomita 84.9, ambapo utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho za maandalizi.
Aidha, amesema upembuzi yakinifu umekamilika na tangazo kwa ajili ya manunuzi ya kupata Wabia linatarajiwa kutolewa Mei, mwaka huu.
More Stories
TFRA yaeleza mbolea ya ruzuku ilivyopunguza gharama kwa wakulima
Serikali yavuna Shilingi Bilioni 3 ndani ya miezi nane
Puma Energy yawataka wakazi wa Dodoma kuchagua nishati safi