March 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkemia Mkuu:Tumedhibiti uingizaji na usafirishaji kemikali hatarishi nchini

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAMLAKA  ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema imeweza kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa kemikali hatarishi na zile zinazodhibitiwa chini ya mikataba ya kimataifa ili kulinda afya ya binadamu, mazingira na usalama wa nchi kwa kutoa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali hizo.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 14 2025 na Mkemia Mkuu wa Serikali,Dkt. Fedelice Mafumiko,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Dkt.Mafumiko amesema Katika kipindi
cha miaka minne cha Serikali ya awamu ya sita kumekuwa na ongezeko la vibali
vya uingizaji wa kemikali kutoka vibali 40,270 kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 hadi vibali 158,820 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 294 ya vibali vilivyotolewa.

“Ongezeko hili la vibali limetokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya
biashara na uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita, wadau kuongeza uelewa wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayosimamia shughuli za kemikali kwa kujengea uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA inayotumika katika uombaji wa usajili na vibali,”amesema Dkt.Mafumiko.

Aidha Dkt.Mafumiko amesema kuwa Mamlaka hiyo imefanya ukaguzi wa Maghala
Katika kuhakikisha kuwa kemikali zinatumika kwa usalama na kwa kufuata taratibu zote zinazohitajika ili kulinda afya ya binadamu na mazingira na pia ili kuhakikisha kuwa kemikali zinazoingizwa nchini ni zile ambazo zinaruhusiwa kisheria kuingia nchini.

“Mamlaka hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maghala yanayohifadhi kemikali na maeneo ya mipaka.Hivyo, katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya awamu ya sita,Mamlaka imefanya ukaguzi wa maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali sawa na
asilimia 119 ya lengo la kukagua maghala 7,160,”amesema Dkt.Mafumiko.

Pamoja na hayo ametaja matarajio ya  Mamlaka hiyo Dkt.Mafumiko amesema kuwa 
inatarajia kupata Hati safi kwa vitabu vya mahesabu vya mwaka wa Fedha
2023/2024 ambavyo ripoti yake inategemea kutolewa mwaka huu wa Fedha (2024/2025).