Na Mose Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.
JESHI la Polisi mkoani Songwe linamshikilia,Mashaka Mwoga (36), mkazi wa Chipaka Mjini Tunduma, wilayani Momba, kwa tuhuma za kumuua mke wake Gloria Anton (32) kwa kumnyonga, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni sababu za wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa alikamatwa Machi 9, 2025, baada ya yeye mwenyewe kuripoti polisi kuwa mkewe ametoweka.
Kamanda Senga amesema kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo, polisi na ndugu wa marehemu walimtilia mashaka mtuhumiwa na kumkamata hadi alipokiri kuhusika na mauaji kisha kwenda kuonesha sehemu alikoutupa mwili wa marehemu huyo.
“Tumebaini kuwa mtuhumiwa alimnyonga mke wake tangu usiku wa kuamkia Machi 8, 2025 na baada ya kufanya kitendo hicho aliazima gari la rafiki yake na kubeba mwili wa marehemu kwenda kuutupa katika shamba la mahindi lililopo kijiji cha Chiwanda, kata ya Nkangamo,” alisema Kamanda Senga.
“Machi 9, 2025, mtuhumiwa alienda kuripoti kituo cha polisi kuwa mkewe ametoweka nyumbani, licha ya kuwa tayari alishamuua.” Alifafanua zaidi Senga.
Kamanda Senga alingeza kuwa,baada ya kuhojiwa kwa kina, alikiri kutenda mauaji hayo na kuonyesha mahali alipoutupa mwili wa marehemu, ambapo Machi 13, 2025, majira ya saa mbili usiku, polisi walifanikiwa kuupata mwili huo ukiwa tayari umeharibika.
“Mtuhumiwa alitumia gari hilo dogo kumbeba marehemu na kwenda kumtupa umbali wa takriban mita 50 kutoka barabara kuu ya Tunduma–Sumbawanga,” aliongeza Kamanda Senga.
Kwa sasa, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Tunduma kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Mtendaji wa Kata ya Chipaka, Cosmas Simwawa, alisema kuwa taarifa za kutoweka kwa marehemu zilianza kusambaa tangu Machi 8, 2025, na ndugu zake walikuwa na mashaka makubwa juu ya kutoweka kwake.
“Awali, polisi walifanya uchunguzi nyumbani kwa marehemu na kukuta shimo lililochimbwa, lakini halikuwa na kitu.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi zaidi, Machi 13, 2025, tulipokea taarifa kuwa mwili wake umepatikana ukiwa umetupwa kwenye shamba la mahindi,” alisema Simwawa.
More Stories
AUWSA yazipatia maji kaya 6000 za kipato cha chini
Daraja la mto Kagatende Suluhisho la Kudumu Utalii na Uhifadhi Serengeti
Mkemia Mkuu:Tumedhibiti uingizaji na usafirishaji kemikali hatarishi nchini