March 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC.Sinyamule mgeni rasmi Misa wadau summit 2025

Na Martha Fatael, TimesMajira Online

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Sinyamule,anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa wadau na waandishi wa habari unaotarajiwa kufanyika Machi 14,2025 jijini Dodoma,ambao umeandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN).

Mkutano huo ni moja ya ndoto ya Misa-Tan katika malengo iliyojiwekea kwenye mkutano wake mkuu wa mwaka jana uliofanyika Desemba 4, jijini Dodoma na kuchagua Bodi mpya ya uongozi, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Edwin Soko.

Ikiwa imebaki siku moja tu kufanyika kwa mkutano Soko, amethibitisha kupatikana kwa wafadhili na ushiriki wa wadau hao kwenye mkutano wa kilele wa MISA na wadau mwaka 2025 (Misa Tan –Wadau SUMMIT 2025).

Soko amesema dhima ya mkutano huo ni kuwaleta pamoja wanachama wa Misa-Tan na wadau mbalimbali,kujadiliana namna ya kutumia nguvu na ushawishi wa vyombo vya habari katika kuchagiza maendeleo.

“Miongoni mwa mambo ya msingi yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na uandishi wa habari wa kujenga, unavyofanyika nchi za Afrika na Tanzania, ushiriki wa vyombo vya habari kwenye uchaguzi mkuu, kanuni, wajibu wa vyombo vya habari pia,”amesema Soko.

Pia amesema mara baada ya kukamilisha MISA-Wadau Summit 2025, kutafanyika kikao cha wanachama cha mrejesho wa masuala mbalimbali yanayohusu taasisi hiyo tangu kufanyika kwa mkutano wake mkuu mwishoni mwa mwaka 2024.

Amesema mkutano huo umefanikiwa baada ya ushirikiano kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Tanzania Human Right Defenders Coalition (THRDC), Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) na Pan African Constructive Journalism initiative (PACJI).

Wadau wengine ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF),Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Hata hivyo,ametoa rai kwa wadau wengine kujitokeza kusaidiana na taasisi hiyo katika kukuza wigo wa ushirikiano na tasnia ya habari nchini, pamoja na kuboresha muhimili wa habari kuelekea uchaguzi mkuu lakini pia mabadiliko ya kidunia ya ukuaji wa teknolojia ili kuimarisha upatikanaji wa habari nchini