*Ni katika sekta ya elimu, afya, miundombinu, maji, kurejesha vyanzo vya mapato H/shauri, afichua siri ya mikeka, Mchengerwa apewa rungu
Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,
Dodoma
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema yote alioahidi kwenye mkutano Mwaka wa Mamlaka ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) wa mwaka 2021 miezi sita baada ya kushika atamu ya uongozi wa nchi ameyatimiza.
Rais Samia alitoa kauli hiyo jijini Dodoma jana wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkutano Mkuu wa 39 ALAT, ambapo alizishukuru mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Serikali Kuu katika kusimamia kazi ambazo zimefanyika.
“Mwaka 2021 nilipozungumza nanyi ilikuwa ni miezi sita tangu nishike atamu ya uongozi wa nchi.
Nilitumia mkutano huo kuainisha mipango ya Serikali kwa wananchi waliopo kwenye halmashauri zetu za wilaya na miji,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alifafanua kwamba aliahidi kujenga jumla ya madarasa 15,000, vituo vya kutolea huduma za afya kwenye tarafa 250, aliahidi kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama na ujenzi wa barabara vijijijini.
Aidha, alisema aliahidi pia kurejesha baadhi ya vyanzo vya mapato vya halmashauri vilivyokuwa vimechukuliwa na Serikali Kuu.
“Sasa ni wajibi wangu kuwarudishia mrejesho wa ahadi hizo, lakini kwa bahati nzuri nilipopita kwenye mabanda ya maonesho kabla sijaingia hapa, majawabu yote niliyakuta na wakurugenzi walinieleza yaliyofanyika,” alisema Rais Samia.
***Elimu
Rais Samia alisema kwenye elimu mbali na kuahidi na kutekeleza ahaadi ya ujenzi wa madarasa 15,000, wamejenga vyuo vya VETA katika wilaya 64 na kazi inaendelea.
Pia alisema vimejengwa vingine 25 na kila mkoa una chuo kikubwa cha mafunzo ya VETA na mafunzo ya ufundi stadi.
***Afya
Kwa upande wa afya, Rais Samia alisema kazi iliyofanyika wanaijua, lakini pamoja na majengo kuna vifaa vya kisasa sana kwenye hospitali zetu katika ngazi zetu.
“Lakini pia tumepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa dawa, usambaza dawa unakwenda vizuri na kuwa rufaa za wagonjwa kwenye Muhimbili na Benjamin Mkapa zinaishia hospitali za mikoa kwa sababu vifaa vyote vipo, wataalam, watumishi kila kitu kiko huko,” alisema Rais Samia.
Aidha, alisema magari ya kuhamisha wagonjwa kutoka hospitali moja kwenda nyingine nayo yapo.
***Maji
Kuhusu maji, Rais Samia alisema wakati ule maji maeneo ya vijijini upatikanaji wake ulikuwa asilimia 80 na 84 mijini.
” Kwa sasa mpaka juzi nilipokuwa nafungua mradi wa Same-Mwanga-Korogwe, vijijini tumetimiza asilimia 83 na lengo tulilopewa ni asilimia 85 .
Na kwenye miji tumefika asilimia 90 tumebakisha tano, kuna miradi zaidi 1,000 maeneo mbalimbali tunapofika Oktoba miradi mingi itakuwa imekamilika, tutafika kwenye agizo tulilopewa na Ilani ya Uchaguzi.”
***Ujenzi barabara za vijijini
Kuhusu eneo hilo, Rais Samia alisema wamejengea TARURA uwezo wa kibajeti na kwa rasilimali watu na hivyo kuiwezesha kufanyakazi zake kwa ufanisi.
Alisema wamejenga barabara mpya za lami, lakini wamefungua barabara nyingi kwa barabara zinazopitika misimu yote, natambua bado kazi ipo ya ujenzi, kila unapokwenda unadaiwa lami na ndiyo raha ya maendeleo,” alisema Rais Samia.
Alisema jambo la faraja wamefungua na Benki ya CRDB, Samia Bond kwa ajili ya fedha za miundombinu hasa barabara.
“Bondi ile tulipoifungua tulikusudia kukusanya sh. bilioni 150 kwa bahati nzuri tumekusanya zaidi ya sh. bilioni 300 hii ni katika kuhakikisha kwamba TARURA haiendi kukwama kwenye utekelezaji wa ujenzi wa barabara vijijini,” alisema.

***Kurejesha baadhi ya vyanzo wa mapato kwenye halmashauri
Kuhusu eneo hilo, alisema makusanyo ya mabango yamerudi kwenye halmashauri, pia wamerudishi ukusanyaji wa kodi ya majengo.
“Kodi hizi zilikuwa zinakusanywa na Serikali za mitaa zikachukuliwa na Serikali Kuu kutokana na ubadhirifu na kutofanya vizuri, sasa tunataka sababu zilizofanya mpokonywe mziondoshe, acheni ubadhirifu na sasa kodi zitakusanywa kwa mifumo,” alisema.
Alisema mambo mengi yamefanyika, lakini suala la umeme kwa wakati ule hawakuliweka kama huduma za jamii, lakini kwa wanavyoenda wanaona ni huduma za jamii na tayari vijiji vyote nchini vina umeme na sasa wanasambaza kwenye vitongoji na baada ya miaka miwili, mitatu Tanzania itakuwa inawaka umeme .
Alisema kuna shida ya kukatika katika kwa umeme na kazi inafanyika , wanajenga njia mpya za kusafirisha umeme, vituo vya kupoza umeme, umeme upo wa kutosha bwawa limekamilika linazalisha megawaiti zaidi ya 2,000 na sasa Tanzania inazalisha megawaiti kama 3,600.
Alisema umeme upo mwingi, tatizo ni kuupeleka na kazi wanaifanya kwa nguvu zote ili Watanzania wapate umeme wa uhakika.
Alisema pamoja na ahadi alizotoa aliahidi changamoto za kufanyia kazi, ambazo ni usimamizi mzuri wa mapato kwa kutumia mifumo ya TEHAMA.
“Lakini ilikuwa kuwachukulia hatua maofisa wabadhilifu na hilo ndilo nililosema mikeka…mikeka, tumechuja tupo asilimia 85. Lakini pia tusema mipango wa halmashauri izingatia vipaumbele vilivyopo katika dira ya Taifa,” alisema
Pia alisema changamoto nyingine ilikuwa ni halmashauri kutenga siku maalum ya kusikiliza kero za wananchi. Alisema eneo hilo bado wanasuasua, ni matumaini yake wataongeza kasi katika utekelezaji.
*** Changamoto za kufanyia kazi zaidi
Alisema changamoto hizo zimefanyiwa kazi, lakini bado kuna changamoto zinahitaji kufanyiwa kazi zaidi,” alisema.
Alitaja changamoto ambazo inafaa washirikiane kuzifanyia kazi, ya kwanza ni katika ukusanyaji mapato na matumizi .
***Aapa kushughulika na mchwa kwenye halmashauri
Rais Samia lisema hadi leo mbali na mifumo ya ukusanyaji mapato, kuna mifumo ya pembeni inatumika kukusanya fedha ambazo zinaingia kwa watu binafsi.
Aliagiza wakurugenzi kuwa macho kwenye eneo hilo, kwani fedha zitakapokusanywa zote zikaingia kwenye mifumo halali, hizo kielele wanazopiga hazitakuwepo.
Alisema wakiziachia zikaingia kwenye mifumo mingine maendeleo yatazorota.
Alimuagiza Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, kama wamebaini hao wanaochepusha fedha katika eneo hilo, lile jicho lake la huruma hapo hapana.
“Wengine pia wamekuja na risiti feki, hao kama mmewangua hapo sina Mswalie Mtume, nitakuja kukuita nikuulize umefanya nini , usipofanya kitu, mimi nafanya kwa wao na wewe,” alisema Rais Samia.
Rais Samia aliipongeza ALAT kwa kazi wanazofanya ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwezo wa watendaji wa halmashauri.
Alisema kufanikiwa kwa mipango ya Serikali Kuu kunategemea sana mamlaka ya Sereikali za Mitaa. Alisema kiasi kikubwa cha fedha za miradi ya maendeleo na miradi ya kuimarisha ustawi wa jamii katika maeneo mbalimbali kinasimamiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Alisema miradi hiyo imechochea maendeleo na kuboresha huduma za kijamii na za kiuchumi kwa wananchi wetu, ndiyo maana mara zote amekuwa akisisitiza uwajibikaji na ufanisi katika halmashauri,kwani huko ndiko waliko wananchi wengi na ndiko wameelekeza miradi mingi ya maendeleo.
Alisema wataendelea kutegemea ushirikiano wao katika kuhakikisha kazi kubwa inayofanywa inaleta matokeo yaliyokusudiwa na kuimarisha ustawi wa wananchi. Alisema ili hayo yatimie kuna mazuri na machungu yake.
*** Kuhusu mikeka
“Mnajua katika kipindi cha miaka mitatu hiki nilikuwa nikitoa mikeka mingine ya mabadiliko,” alisema. .
Alisema amekuwa akitoa mikeka hiyo siyo kwa raha wala kwa kupenda, bali kwa kutafuta walio safi watakaosimama na Serikali kufanyakazi ambayo imekusudiwa na Serikali.
“Sasa nataka kusema kwamba kama maksi ni 100 tupo kwenye 85, tumeisha nyooka , tumebakiza 25 tutakwenda kunyoshana pole pole mpaka wote tusimame njia moja,” alisema Rais Samia.
More Stories
NaCoNGO yazindua kikosi kazi cha ukusanyaji maoni
Dkt.Biteko awasili Barbados kunadi nishati safi kimataifa
Jamii yatakia kuacha matumizi hole la ya dawa ili kuepuka kupata ugonjwa wa figo