March 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Madini yafungu kamfanikio uongozi wa Samia

Na Joyce Kasiki, Timesmajira, Dodoma

TUME ya Madini nchini imetaja mafanikio yake kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa ni pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na rasilimali madini, kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu miaka minne ya Dkt.Samia, Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Mhandisi Ramadhan Lwamo alisema ,kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka sh. bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia sh. bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Alisema,makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu huku akisema,katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Februari, 2025, Tume imefanikiwa kukusanya jumla ya sh. 690,763,401,639.06 sawa na aslimia 69.08 ya lengo la Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Aidha alisema mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023.

” Hii ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za Madini.”alisema Mhandisi Lwamo

Vilevile alisema,ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023 ambapo kutokana na kuendelea kuimarika kwa Sekta ya Madini, mwenendo wa Mchango wa Sekta ya Madini na ukuaji wake unatarajiwa kufikia asilimia 10 na zaidi ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Kwa mujibu wa Mhandisi Lwamo, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini iliendelea kusimamia utendaji kazi wa Masoko ya Madini na vituo vya ununuzi wa Madini nchini.

Alisema,hadi kufikia Februari, 2025 , Tume ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , imefanikiwa kuanzisha masoko 43 na vituo vya ununuzi 109 ambapo kuanzia Mwaka wa Fedha 2021/2022 mauzo ya madini katika Masoko na Vituo vya Ununuzi wa madini yameendelea kuongezeka kutoka Shilingi 2,361.80 bilioni hadi Shilingi 2,597.18 bilioni kwa Mwaka 2023/2024.

“Mauzo hayo yamesababisha Tume ya Madini kukusanya maduhuli ya Serikali. Maduhuli hayo yanatokana na Mrabaha na Ada ya Ukaguzi wa madini yaliyouzwa kwenye Masoko na Vituo vya Ununuzi wa madini.”

Aidha alisema,Tume ya Madini katika kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini, wasambaza bidhaa na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.

Katika hatua nyingine Mhandisi Lwamo alisema ,Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi rejewa, Tume imefanikiwa kutenga maeneo 58 kwa ajili ya Wachimbaji wadogo katika Mikoa mbalimbali nchini.

Vile vile alisema,Tume imeendelea kuwatengenezea mazingira rafiki kwa ajili ya kupata leseni za uchimbaji pamoja na kuwaunganisha na Taasisi za kifedha ili wapate mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za uchimbaji.

“Pia, Tume ya Madini imeendelea kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kijiolojia Tanzania (GST) katika kuyafanyia utafiti maeneo mbalimbali ili kuwawezesha Wachimbaji kupata taarifa sahihi za uwepo wa rasilimali Madini na kufanya uchimbaji wenye tija.”alisema na kuongeza kuwa

“Tume ya Madini imekuwa ikitoa leseni za uendeshaji wa shughuli za madini kwa wadau wake kwa kuzingatia Sheria ya Madini Sura 123. Ili kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, katika kipindi cha kuanzia 2021/2022 hadi kufikia Januari 30, 2025, Tume imefanikiwa kutoa jumla ya leseni 41,424 kati ya 37,318 sawa na asilimia 111. “

Alisema Leseni hizo zilijumuisha leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini. Jedwali Na. 4 linabainisha mgawanyo wa leseni zilizotolewa.

Katika hatua nyingine alisema, Tume imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Madini nchini kwa kutoa leseni kubwa kwa Kampuni mbalimbali za uchimbaji.

Mhandisi Lwamo alisema , leseni hizo za uchimbaji mkubwa wa Madini zilitolewa kwa kampuni mbalimbali kuanzia Mwaka 2021 hadi Januari, 2025 ambapo utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa katika Sekta ya Madini pamoja na Sekta nyingine fungamanishi hapa nchini.