April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikh Mustafa awataka wanaofuturisha kuiga mfano wa Rais Samia

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma

SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma Alhaj Mustafa Rajabu amewataka wale wanaofuturisha katika mwezi wa Ramadhan kufuturisha watu wenye mahitaji na kuacha kufanya ibada hiyo kwa watu wanaojiweza.

Huku akiwataka kuiga mfano wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kama alivyofanya hivi karibuni Ikulu Jijini Dar es salaam kufuturu nao wale wenye uhitaji.

Sheikh Mustafa  ametoa kauli  hiyo  Leo Ijumaa Machi 7,2025 wakati akitoa mawaidha ya katika ibada ya swala ya Ijumaa katika msikiti wa Gaddafi Jijini hapa.

Amesema inashangaza baadhi ya Taasisi,kampuni,Wizara na wafayabiashara wakubwa kufuturisha watu wasiokuwa na mahitaji kitu ambacho siyo maelekezo ya dini ya Kiislam kama ilivyo kwenye Qur’an.

“Hili wewe muislamu unalijua?leo hii futari zetu tunawaalika watu ambao hawana haja na futari zetu leo wanajigamba umewafuturisha kina nani.

Hao uliowafuturisha tunauhakika wanaihitaji kuna watu wanafuturu maji meseji hii iyafikie makampuni,Taasisi wanaostahiki kufuturishwa ni wale ambao hawana uwezo.

“Wale wajane ambao walikuwa wana waume zao,lakini leo unamwita mtu ana uwezo Waziri Mbunge,Injinia hatukatai kufanyiana wema lakini lazima muangalie wenye mahitaji.

“Kuna watu wanamahitaji makubwa,ndugu zangu tumuigeni Rais wetu ibada ya swaumu kwa kuanza na wale wenye mahitaji tuige mfano.Ndugu zangu mema yote haya tutakayoyafanya tutaingizwa katika Mlango na kuona Yale tuliyoyafanya,”amesema Sheikh Mustafa.

Sheikh Mustafa amesema kama ulimkosea Mwenyezimungu huu ndio muda wa kutubu na kutumia fursa ya Afya na uzima kuhakikisha wanautendea haki.

“Huu ni mwezi wa kusameheana kuunganisha undugu.Ramadhan ni mwezi wa kusimamia na kisimamo Cha Taraweeh.Ibada hii imekuja kukutengeneza kimwili na kimaumbile,ile itakupa nafasi ya kufanya mazoezi na kupata thawabu,”amesema Sheikhe Mustafa

Amesema Ramadhan ni mwezi wa kutenda mema,kutoa sadaka na thawabu zake ni kubwa na mara dufu.