Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MFUKO wa Utamaduni na Sanaa Tanzania umesema katika mwaka wa fedha 2024/25 bajeti ya mfuko huo imeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 3 kutoka bilioni 1.6 mwaka wa fedha 2023/24.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 28,2025 na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa,Tanzania Nyakaho Mahemba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mfuko huo katika miaka minne ya serikali ya awamu ya sita ambapo amesema kiasi hicho kilichoongezeka ni Shilingi Bilioni 1.4 ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 87.5.
“Haya yote yamewezekana kutokana na Uongozi mahiri na madhubuti wa Rais Wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wakiwa na lengo la kuinua ubora wa kazi za Utamaduni na Sanaa ili ziweze kujiendesha kibiashara, kuzalisha ajira pamoja na kuchangia katika pato la Taifa,”amesema Nyakaho.
Nyakaho amesema Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa Mfuko katika ukuzaji na uendelezaji wa miradi ya Sanaa ili iweze kuzalisha bidhaa bora na shindani kulingana na viwango na mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi,ilichukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuongeza bajeti ya Mfuko ili uweze kutekeleza majukumu yake ya Msingi hususani katika kuzalisha ajira na kuongeza fedha za kigeni.
Aidha amesema Serikali imeongeza chanzo kipya na endelevu cha mapato ya Mfuko kinachotozwa katika vibebeo tupu vya Kazi za Sanaa (Tozo ya Hakimiliki – Copyright Levy). Aidha, kupitia chanzo hichi, Mfuko hupata gawio la asilimia 10 ya mapato yote yanayokusanywa ambacho kimeanza kutekelezwa Mwezi Septemba,2023.
Vilevile Nyakaho amesema Mfuko huo unatoa mikopo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB na NBC lengo la ushirikiano huo ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kutumia utaalamu na uzoefu wao katika eneo la utoaji wa mikopo, usimamizi wa marejesho pamoja na ufuatiliaji wa miradi iliyowezeshwa.
Nyakaho amesema Mfuko huo umefanikiwa kutoa Mikopo yenye thamani ya Shilingi 5,250,070,500.89 kwa miradi 359 ya Sanaa iliyozalisha jumla ya ajira 497,213.
“Maeneo ya miradi ya iliyowezeshwa ni muziki,miradi 78, filamu miradi 90, maonesho miradi 65,Ufundi  miradi 103 na Lugha na Fasihi 23 na
Mikoa iliyofikiwa ni 18 ambayo ni Dar- Es Salaam, Arusha, Morogoro, Pwani, Geita, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Simiyu, Kigoma na Katavi,”.amesema.



More Stories
Katibu Mkuu Nishati aipongeza Sweden kufadhili miradi ya umeme nchini
RAS Seneda akabidhi msaada wa Mablanketi kwa wazee na yatima
Balozi Nchimbi:Mapambano ya uhuru wa kiuchumi Kusini mwa Afrika yanaendelea