Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imefanikiwa kukusanya sh. 178,363,295,697 kwa kipindi cha miezi sita kutoka Julai 24 hadi Desemba 24, 2024 sawa na asilimia 109 ya lengo walilojiwekea la sh. 162,936,698,960.
Ongezeko hilo ni sh. 82,850,757,764 sawa na asilimia 87 ya makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2023/2024, kwani kuanzia Julai 23 hadi Desemba 23, 2023, lengo ilikuwa kukusanya sh. 108,675,013,758, lakini waliweza kukusanya sh. 95,512,597,934 sawa na asilimia 88.

Hayo yamesemwa Februari 21, 2025 na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Thomas Masese alipokuwa anazungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya semina iliyoandaliwa na TRA kwa ajili ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Korogwe, kutoa elimu kwa mlipa kodi iliyofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe.
“Katika mwaka wa fedha 2024/2025 katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 24 hadi Desemba 24, 2024, lengo ilikuwa kukusanya sh. 162,936,698,960, lakini tuliweza kukusanya sh. 178,363,295,697 sawa na asilimia 109.
“Ongezeko hilo ni sh. 82,850,757,764 sawa na asilimia 87 ya makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2023/2024, kwani kuanzia Julai 23 hadi Desemba 23, 2023, lengo ilikuwa kukusanya sh. 108,675,013,758, lakini tuliweza kukusanya sh. 95,512,597,934 sawa na asilimia 88” alisema Masese.
Masese alisema wameweza kupata mafanikio hayo makubwa kutokana na kutoa elimu kwa walipa kodi kwa kuzunguka kwenye wilaya zote nane (8) za Mkoa wa Tanga, na kuwaeleza umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, huku wakisikiliza changamoto mbalimbali za wafanyabiashara.

“Leo tupo hapa wilayani Korogwe katika zoezi la kutoa elimu kwa walipa kodi wetu. Zoezi hili tunafanya kwa kushirikiana na vyama vya wafanyabiashara, tunafanya na TCCIA (Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo), na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT). Zoezi hili tumelifanya kwa Wilaya ya Mkinga, Muheza, Mkata (Handeni), Kilindi, na sasa Korogwe, na nia ni kufanya wilaya zote za Mkoa wa Tanga.
“Nia ya kufanya ziara hii ni katika kuongeza uelewa kwa walipa kodi wetu ili waweze kulipa kodi vizuri, lakini pia ni katika kuongeza mahusiano kati ya mamlaka ya mapato, walipa kodi, lakini na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara. Katika semina hii tunapata nafasi ya kutoa wasilisho (mada) ya mambo ya kulipa kodi, lakini pia tunatoa nafasi ya kusikiliza maswali, maoni na ushauri kutoka kwa walipa kodi wetu kwa jinsi ambavyo tunawapa huduma” alisema Masese.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Masese aliwasisitiza kuwasilisha ritani zao, lakini pia kipindi hiki ni cha makadirio, na kilianza Januari mosi, na kitamalizika Machi 31. Hivyo, wafanyabiashara wote wanaostahili kufanya makadirio, waweze kufanya hivyo kwa kufika Ofisi za TRA. Lakini kwa wale wanaostahili kuwa na mashine za risiti za kielektroniki (EFD), waweze kununua mashine hizo ili kupata mauzo sahihi ambayo yatasaidia katika ukadiriaji wa kodi.

Pia wale wafanyabiashara wanaostahili kusajiliwa kwenye mfumo wa Ongezeko la Thamani (VAT) waweze kufanya hivyo. Na kwa wale wenye madeni wanatakiwa walipe kwa wakati, lakini wenye madeni makubwa wafike Ofisi za TRA na waweze kujadiliana, na wakikubaliana basi waombe kulipa kidogo kidogo.
Wakieleza changamoto zao, mfanyabiashara Anna Munuo kutoka Kijiji cha Makuyuni, Kata ya Makuyuni ambaye anauza nguo kama mfanyabiashara mdogo, amewataka TRA wafike ili kuona biashara zao, kwani kukadiriwa wakiwa Ofisi za TRA hawatapata makadirio halisi, na yanaweza kuwaumiza wao wafanyabiashara.
Naye Anna Mzoo wa Mtaa wa Mlimafundi eneo la Mountain View mjini Korogwe, alisema yeye ni mwenye duka la rejareja anaelipa kodi, lakini kuna maduka madogo madogo yameanzishwa kwenye mtaa wao, lakini hawalipi kodi TRA wala leseni Halmashauri ya Mji Korogwe.

More Stories
Waislamu Mwanza wapokea Ramadhani kwa maandamano ya kidini
Kamati ya kudumu ya Bunge ya utawala,katiba na sheria yaridhishwa ujenzi soko Kariakoo
Wataalam Sekta ya utalii watakiwa kufanya kazi kwa uadilifu,kujituma na kuwa wabunifu