Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watuhumiwa 21 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuingiza mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na Serikali kuingizwa na kutumika nchini,utapeli wa viwanja, kughushi nyaraka za umiliki na vyeti vya udereva.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Naibu Kamishna Wilbrod Mutafungwa, amesema hayo Februari 20,2025,ambapo katika kipindi cha Januari 20 hadi Februari 20,mwaka huu ,watuhumiwa hao wamekamatwa kwa tuhuma mbalimbali,zikiwemo za kuingiza mifuko ya plastiki kinyume cha sheria,utapeli wa viwanja,kughushi nyaraka na vyeti vya udereva.
Akizungumzia tukio la kukamatwa kwa mifuko ya plastiki Mutafungwa ameeleza jinsi polisi walivyofanikiwa kukamata mfanyabiashara, Stanslaus Chacha (22), mkazi wa Guta, wilayani Bunda na Byabato Gidion (34),mvuvi na mkazi wa Misenyi mkoani Kagera, wakiingiza mifuko ya plastiki 165, ingawa serikali ilishapiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo nchini.
Amesema mifuko hiyo ilikamatwa wakati wa operesheni iliyoendeshwa katika maeneo ya Nyangulugulu, wilayani Ilemela, ambapo watuhumiwa walikamatwa ndani ya Ziwa Victoria, wakiwa na mtumbwi wenye namba za usajili 01245,MV KABULA I uliokuwa ukisafirisha bidhaa hiyo kupitia ziwa hilo.
Mutafungwa amesema tukio jingine la uhalifu ni pamoja na Biglister Mbowe, mfanyabiashara maarufu, ambaye alikamatwa kwa tuhuma za kughushi nyaraka za umiliki wa viwanja na kuwauzia watu akijifanya mmiliki halali.
Amesema mtuhumiwa huyo akishirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na vitongoji, alighushi nyaraka za umiliki wa kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 480 akakiuza kwa Hamis Abdallah (32) ambaye ni mwandishi wa habari, baada ya kujifanya Frola Kasambala, mwenye hati ya mauziano.
“ Hii ni ishara ya kuongezeka kwa changamoto za migogoro ya ardhi,watu wanajifanya kuwa na nyaraka halali ili kufanikisha udanganyifu (utapeli) na kujipatia fedha.Biglishter anashirikiana na viongozi wa serikali za mitaa wasio waadilifu wakitumia nafasi zao kuaminisha wanunuzi kuwa maeneo hayo anayamiliki kihalali,”amesema Mutafungwa.
Amewataja wengine katika kadhia hiyo ni Mwenyekiti na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Nyakalekwa,Kata ya Luchelele Yohana Kilango (45) na Mohamed Omari (52), Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwabogoso,Kata ya Kisesa,Magu, Joas Kimbulu (32), mjasiriamali na mkazi wa Nyasaka, Ilemela, Salome William (26), na Benedicto Mathias (50),dalali wa viwanja na mkazi wa mtaa wa Nyamatara,Kata ya Buhongwa,Nyamagana.
Hata hivyo,amesema kupitia ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama, polisi wamegundua mtandao mkubwa wa uhalifu huo ambao umekuwa chanzo cha migogoro katika jamii na familia wakati mwingine kusababisha mauaji .
Katika hatua nyingine, operesheni hiyo pia imeangazia tatizo la kughushi vyeti vya udereva, ambapo watuhumiwa nane wamekamatwa kwa kughushi vyeti vya udereva ili kuvitumia isivyo halali kuongeza madaraja katika leseni zao.
Mutafungwa amesema Februari 17, mwaka huu, majira ya saa 6:30,katika ofisi ya Mkuu wa Usalama Barabarani,Mkoa wa Mwanza (RTO),alikamatwa Denis Lucas (38),dereva na mkazi wa Bugakama, wilayani Kwimba akiwa na vyeti vya kughushi akivitumia kuongeza madaraja katika leseni yake.
Pia,watuhumiwa wengine nane walikamatwa kwa kosa la kughushi vyeti vya udereva vilivyotolewa na Chuo cha VETA pamoja na barua za uhakiki wa leseni kutoka kwa RTO.
Amewataja watuhumiwa hao ni Ofisa Masoko wa Chuo cha Ufundi Sengerema,Jumbura Manumbu (42)na Philimo Okoth (54),wakazi wa Kisesa na Bukandwe,wilayani Magu,Samwel Bose (47),Mohamed Ismail (36) na Agnes Dionizi (31),wote wakazi wa wilayani Ilemela,Gatahwa Sawawa (27),mkazi wa Sengerema na Sethbenjamin Mpory (43),mkazi Ngudu,Kwimba.
“Watuhumiwa wote wamehojiwa na watachukuliwa hatua za kisheria,Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kufuata taratibu za kupata leseni za udereva kwa kusoma na kupata mafunzo katika vyuo vya VETA,kisha kuhakikiwa na polisi kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu za usalama barabarani,”amesema.
More Stories
Wataalam Sekta ya utalii watakiwa kufanya kazi kwa uadilifu,kujituma na kuwa wabunifu
Shigongo: Rais Samia ameleta mafanikio mengi katika kukuza uchumi
Mpogolo amahukuru Dkt Samia