February 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakama yathibitisha mshitakiwa mauaji ya Asimwe hana tatizo la akili

Na Ashura Jumapili TimesMajira online Kagera,

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba imethibitisha kuwa aliyekuwa Padri Elpidius Rwegoshora hana tatizo la afya ya akili baada ya kupokea ripoti kutoka Hospitali ya Isanga Dodoma iliyosainiwa na Daktari wa hospitali hiyo.

Ambapo ripoti hiyo imethibitisha kuwa mshitakiwa huyo wa kesi ya mauaji namba 25513 ya mwaka 2024, ya mtoto mwenye ualbino Noela Asimwe Novath inayowakabili watuhumiwa tisa akiwemo aliyekuwa Padri Rwegoshora hana changamoto ya afya ya akili.

Hayo yameelezwa Februari 17,2025 na Jaji wa Mahakama hiyo, Gabriel Malata mbele ya Mahakama kabla ya usikilizwaji wa shauri la kesi ya mauaji ya mtoto Asimwe katika Mahakama hiyo kwa hatua ya awali.

Jaji Malata,amesema kuwa ombi hilo liliwasilishwa na upande wa utetezi wa mshtakiwa namba moja mnamo Oktoba 25, 2024 na Mahakama kuridhia na kutoa amri mshtakiwa huyo kupelekea hospitali ya Isanga kwa ajili ya vipimo.

Amesema baada ya kufanyika kwa vipimo, taarifa ya vipimo hivyo imesainiwa na kudhibitisha majibu hayo na daktari Enok Changalawe, na tayari nakala za majibu zimekabidhiwa kwa Mawakili wa mashtaka na utetezi.

Jaji Malata akisoma taarifa hiyo amesema kuwa “Bwana Elpidius Rwegoshora hajaonesha dalili yoyote ya kuwa na ugonjwa au matatizo ya akili na kuwa suala la kutokuwa na akili timamu halikubainishwa kitabibu,”.

Kwa upande wa Jamhuri Wakili wa mashtaka wakiongozwa na Wakili wa Serikali Ajuaye Bilishanga pamoja na Agness Awino na Matrida Assey,wameeleza kuwa kielelezo hicho cha taarifa za vipimo kitumike katika shauri hilo kwa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Aidha, Mshtakiwa namba tatu Nurdin Masoud amekana jina hilo kuwa sio jina lake licha ya kukiri mbele ya Mahakama kuwa yupo mahakamani hapo kama mshtakiwa namba tatu na kusomewa shtaka.

Katika kesi hiyo leo mshtakiwa namba moja amesimamiwa na Mawakili wa utetezi watatu lakini mshtakiwa namba mbili hadi tisa wamesimamiwa na Wakili mmoja Projestus Mulokozi .

Washtakiwa wote tisa akiwemo aliyekuwa Padri wa Kanisa Katoliki Elpidius Rwegoshora na baba mzazi wa Asimwe, Novath Venant wamesimama kizimbani mbele ya Jaji Malata.

Washtakiwa wote tisa wamesomewa shtaka la kuua kwa kukusudia kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya 196 na 197 ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022, na wote kukana shtaka hilo.

Katika kesi hiyo jumla ya hoja 21 za kubishaniwa na kutobishaniwa zimeibuliwa katika Mahakama hiyo na mawakili wa Serikali.

Baada ya kusikilizwa kwa shauri hilo hatua ya awali, Mahakama imetamka kwamba usikilizwaji umekamilika na sasa inaenda kusikilizwa kesi ya msingi.

Katika kesi ya msingi kwa upande wa Jamhuri wameorodhesha jumla ya mashahidi 52, vielelezo vya maandishi 27 na vielelezo halisi 10

Jaji Malata ameelekeza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kupanga tarehe na namna ya usikilizwaji wa shauri hilo.