Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
WAGANGA wa Tiba Asili wametakiwa kuacha kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani kwa kufanya hivyo kunawapaka matope waganga hao, lakini pia kunawaweka hatarini kufungwa maisha na kuacha familia zao zikitaabika.
Hayo yamesemwa Februari 16, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waganga na Wakunga wa Tiba Asili Tanzania (CHAWATIATA) Mkoa wa Tanga, Zuberi Sayavuli kwenye semina ya siku moja iliyowashirikisha Waganga wa Tiba Asili Tarafa ya Korogwe, na kufanyika Ukumbi wa CCM mjini Korogwe.

Sayavuli pia aliwataka Waganga wa Tiba Asili waache kutumia njia ovu ya kuwateka watu hasa watoto kwa ajili ya kuwakata viungo kwa minajili ya kidai vinawasaidia wanasiasa kupata uongozi.
“Waganga wa Tiba Asili mnatakiwa kuacha kabisa kujihusisha na usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya. Jambo hilo ni hatari sababu, kwanza linavunja uaminifu na kuona sisi waganga wote tunajihusisha na dawa za kulevya. Lakini pia jambo hilo linakufanya wewe uweze kupotea kwa kufungwa na kuacha familia yako.
“Lakini pia tuache kujihusisha na utekaji wa watu hasa watoto kwa ajili ya kuwatoa viungo na kudanganya kuwa kiungo cha binadamu kinamsaidia mtu kupata uongozi. Hayo ni mambo mabaya ambayo hatutakiwi kujihusisha nayo” alisema Sayavuli.
Katibu Mkuu wa CHAWATIATA Mkoa wa Tanga Juma Kaoneka amewataka Waganga wa Tiba Asili kuacha kufanya udhalilishaji hasa kwa wanawake, kwani baadhi ya waganga, wanawavua nguo zote wateja wao, na hasa wanawake ili waweze kuwatibu.

“Mnatakiwa kuacha vitendo vya kuwadhalilisha wagonjwa wenu. Hili jambo wanafanyiwa sana wanawake, kwani baadhi yenu mnawaeleza wavue nguo zote ili muweze kuwaingizia dawa. Kitendo hiki hakikubaliki, na kinawaondolea uaminifu na kufukuza wateja wenu” alisema Kaoneka.
Katibu wa Tiba Asili Kata za Majengo na Manundu mjini Korogwe Ustaadhi Masha Mwelekwa alisema Serikali isitoe vibali ama vyeti kwa Waganga wa Tiba Asili ambao hawajajiunga na CHAWATIATA, kwani kwa kufanya hivyo wanaingiza matapeli kwenye fani hiyo, na kujihusisha na vitendo viovu ikiwemo dawa za kulevya na kuteka watoto kwa ajili ya kuwakata viungo.
Mtaalamu wa Tiba Asili kutoka Mtaa wa Kwameta, Kata ya Kwamndolwa, Halmashauri ya Mji Korogwe Ramadhan Sheshe, alisema waganga matapeli ni wale ambao hawajajiunga na CHAWATIATA, hivyo kuwe na msako mkali wa kubaini watu hao ili kurudisha imani kwa Serikali na jamii kuwa Waganga wa Tiba Asili ni watu waadilifu na waaminifu kwenye jamii.
Katibu Mwenezi wa CHAWATIATA Wilaya ya Korogwe Yusuph Singano aliwataka viongozi wa chama hicho ngazi ya kata kuwa walinzi wa kuwabaini waganga matapeli waliopo kwenye maeneo yao, kwani wao ndiyo rahisi kuwabaini watu hao.
“Ninyi viongozi wa kata ndiyo mnatakiwa kutusaidia kuwabaini waganga waliovamia fani hiyo na kuendesha shughuli zao kitapeli huku wakijihusisha na vitendo viovu ikiwemo dawa za kulevya” alisema Singano ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mombo wilayani Korogwe.
Katibu wa CHAWATIATA Wilaya ya Korogwe Nicodemus Mwajombe alisema wao kama viongozi ngazi ya wilaya, wapo makini kuweza kumkamata mganga yeyote anaevunja sheria na kumfikisha kwenye vyombo vya dola kabla sheria haijachukua mkondo wake, kikubwa wapewe taarifa na wananchi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kikao, Sayavuli alisema kama viongozi wa CHAWATIATA Mkoa wa Tanga, wamepewa jukumu na Serikali la kutoa elimu kwa Waganga wa Tiba Asili kwenye mkoa huo ili waache kujihusisha na vitendo viovu.
“Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ametupa jukumu sisi viongozi wa CHAWATIATA kwa kututaka wenyewe kwa wenyewe tupeane elimu ya kuachana na mambo mabaya, kwani imebainika baadhi ya waganga wanatumia tunguli zao kusafirisha dawa za kulevya, na utekaji wa watu, na katika waliowahi kukamatwa, baadhi yao ni waganga kutoka Tanga.
“Hivi unavyotuona hapa Korogwe, tayari tumeshatoa elimu kwenye wilaya tano za Tanga, Mkinga, Handeni, Lushoto na Korogwe. Bado Muheza, Kilindi na Pangani, ikiwa ni muendelezo wa kutoa elimu hiyo” alisema Sayavuli.

More Stories
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Baraza la Taifa la Ujenzi waingia makubaliano ya mashirikiano sekta ya ujenzi
Nderiananga aongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu ujerumani
Taarifa za maendeleo ziwafikie wananchi kwa usahihi