February 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulega atangaza neema ya Samia kwa wakandarasi

Walipwa zaidi ya bilioni 254/- ndani ya siku 60,
lengo ni kumalizia miradi ya barabara, madaraja

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali imelipa takribani sh. bilioni 254 ndani ya miezi miwili kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya barabara na madaraja nchini baada ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ulega aliyasema hayo jijini Dodoma jana mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Ntyuka hadi Kikombo yenye urefu wa kilomita 76 inayojengwa kwa awamu mbili na wakandarasi wawili ambao ni CHICO pamoja na China First.

Waziri huyo alisema Rais Samia ametoa maelekezo ya kulipwa kwa wakandarasi hao, ili kuwajengea uwezo wa kukamilisha miradi yote ya sekta ya ujenzi kutekelezwa kama ilivyopangwa.

“Mmeona katika muda wa hii miezi mwili, Rais Samia tayari amelipa malipo ya wakandarasi ya takribani shilingi bilioni 254, matumaini yetu tunataka kuona kazi zikiendelea “, amesema Ulega.

Ulega aliongeza kuwa mwishoni mwa Februari mwaka huu, Serikali inatarajia kutoa fedha nyingine za kutekeleza miradi ya miundombinu katika sekta ya ujenzi ambapo ameiagiza TANROADS kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ianze kujengwa haraka.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema kuwa barabara ya Ntyuka – Mvumi- Kikombo ni barabara ya kihistoria hivyo ameomba Serikali kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani ni mkombozi kutokana na uwepo wa hospitali kubwa ya macho ya MVUMI inayotoa huduma nchi nzima na pia kuunganisha maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi, Mohammed Besta amesema kuwa Ujenzi wa barabara ya Ntyuka – Mvumi- Kikombo unatekelezwa kwa Sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza kutoka Ntyuka- Mvumi- Makulu na Kikombo – Chololo -Mapinduzi (Km 25) inatekelezwa na Mkandarasi CHICO kwa gharama ya shilingi Bilioni 38.1 na sehemu ya Pili ya Ntyuka -Mvumi Hospitali – Kikombo (Km 53) inatekelezwa na Mkandarasi China First kwa gharama ya sh. Bilioni 98.4.